Na Andrea Ngobole, maipac
Kituo cha utafiti wa masomo ya Tabianchi na mazingira cha chuo kikuu Cha
Aga Khan kilichopo jijini Arusha kimezishauri nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) kuongeza idadi ya viwanda vinavyozalisha bidhaa
zisizoharibu mazingira na kufyonza kaboni kwa Maendeleo Endelevu (SDGs) ili
kuwalinda binadamu, mimea na mifugo isipate madhara ya mabadiliko ya tabia
nchi.
Mkurugenzi wa kituo hicho Dkt. Emmanuel Sulle ameyasema
hayo katika ziara maalumu ya waandishi wa Habari za mazingira walipotembelea
kituo hicho hivi karibuni kwa ajili ya kujifunza namna bora ya kutatua
changamoto za athari za mabadiliko ya Tabianchi, uhifadhi bora wa mazingira na
kudhibiti hewa ukaa.
Alisema endapo nchi za jumuiya ya Afrika mashariki
zikiongeza zaidi viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali kwa kutumia nishati
safi basi mazingira yatakuwa bora na wananchi watanufaika na ajira, utunzaji wa
miti utakaowezesha uvunaji wa bayoanuwai na kufyonza kaboni ili kulinda
mazingira.
Taasisi hiyo imejikita zaidi katika utafiti wa kutatua
changamoto za mazingira kwa jamii kwa kuwawelimisha uzalishaji wa mazao
mchanganyiko ili kufanikiwa kupata mazao na chakula cha kutosha kwa ajili ya
familia na kuongeza kipato cha familia kwa kuuza mazao hayo.
“Elimu ya ukombozi nimuhimu sana kwa ajili ya kuleta mabadiliko
ya Uchumi wa familia na jamii kwa ujumla” Alisema Dkt. Sulle
Amesema jamii zinazoishi ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania
ni jamii zinazoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi kutokana na ukame hivyo ni
lazima wapande miti na majani yanayohimili ukame na upatikanaji wa malisho ili
kuinua uchumi na kuondokana na changamoto za mmomonyoko wa udongo.
Alisema katika karne ya 21 elimu ya kukabiliana na
mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi si ya kukaa darasani pekee
lazima sasa wanafunzi watekeleze kwa vitendo ili kuhakikisha mazingira
yanatunzwa ndio maana taasisi hiyo inashirikiana na jamii kwa kupata maarifa ya
asili katika utunzaji wa mazingira ikiwemo mifugo.
"Katika taasisi hii tunayo miti zaidi ya 75 aina
tofauti tofauti ikiwemo mti wa mpingo na tukiamua kuongeza viwanda lazima tujue
vinazalisha bidhaa zisizo haribu mazingira lakini endapo ushirikishwaji wa
utunzaji mazingira utashirikisha wanafunzi ngazi za chini utawasaidia kuwa
mabalozi wa kuleta mabadiliko ya kweli" Alisema Dkt. Sulle
Alisema mabadiliko ya tabia nchi yanaleta athari kubwa kwa
wananchi waliopo pembezoni hivyo kila mmoja anapaswa kulinda mazingira ili
kuepukana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuongeza kuwa mwaka huu nchi za
Kenya na Tanzania zilipata athari ya mafuriko ya mvua kubwa kunyesha na
kuharibu mazingira lakini sababu kubwa baadhi ya maeneo hayapo katika hali ya
uhalisia kutokana na ukatwaji wa miti na udongo kutokana na shughuli za
kibinadamu.
Alisisitiza upandaji wa miti zaidi katika maeneo mbalimbali
ili kuvuta hewa nzuri na kuondoa magonjwa mbalimbali yanayotokana na mabadiliko
ya hali ya hewa na kuachana na kilimo kisicho endelevu ikiwemo kutumia nishati
mbadala kama vile gesi asilia inayopunguza uchafuzi wa mazingira ikiwemo
matumizi ya sola.
Naye Mkurugenzi wa Kampasi ya Aga Khan Arusha, Murad
Jivan alisema wanashirikiana na jamii katika kuhakikisha utunzaji wa mazingira
ikiwemo upandaji wa miti, upandaji wa maua, kilimo cha majani kwaajili ya
malisho ya mifugo ili kuwezesha wafugaji kuondokana na migogoro baina ya
wakulima na wafugaji kutokana na ukosefu wa malisho unaosababishwa na shughuli
za kibinadamu.
No comments:
Post a Comment