MBUNGE KAWAWA AJENGA SHULE YA SEKONDARI, AONDOA ADHA YA WANAFUNZI KUTEMBEA UMBALI MREFU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 18 July 2024

MBUNGE KAWAWA AJENGA SHULE YA SEKONDARI, AONDOA ADHA YA WANAFUNZI KUTEMBEA UMBALI MREFU

 




Na Mwandishi wetu. Namtumbo

maipacarusha20@gmail.com


Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, Vita Kawawa katika kuhakikisha anaondoa adha ya kutembea umbali wa kilometa. 15 kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Msisima amejenga shule karibu na maeneo wanayoishi.


Baada ya kujengwa kwa shule wanafunzi hao walimshukuru Mbunge huyo na kueleza kuwa Sasa watasoma kwa usalama zaidi.


Akizungumza na waandishi wa habari,walipotembelea shuleni hapo wakati wa ziara ya Mbunge huyo,Mwanafunzi wa kidato cha kwanza shuleni hapo Ikram Abdallah alisema, awali wanafunzi  waliotangulia walishindwa kumaliza masomo na baadhi walifeli kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda shule.


Wanafunzi wa shule hiyo walikuwa wakilazimika kufuata masomo umbali huo na kwenda kusoma kata jirani ya Lusewa kwani wanafunzi  wengi walishindwa kumaliza masomo kwa kushawishiwa na kupata ujauzito,na kuumizwa na wanyama wakali .


Kwa upande wake mwanafunzi Huzuni Mgomba alisema kujengwa kwa shule hiyo kumepunguza manyanyaso hasa kwa watoto  wakike ambao walikuwa wakilazimishwa kushiriki ngono na vijana wa boda boda na wengi wakaishia kupata mimba za utotoni  na kuishia kuharibu maisha yao.


"Tunamshukuru Mbunge kwa kushirikiana na wazazi  walianzisha ujenzi wa shule hii kwa kujitoa kidogo kidogo ili sisi tuweze kusoma kwenye maeneo karibu  na nyumbani na baadaye Rais Samia akaleta pesa kumalizia ujenzi wa shuke yetu hivyo tunawashukuru sasa tunasoma kwenye mazingira mazuri na tunapata elimu bora ambayo itatuwezesha kufanya vizuri kwenye mithiani yetu,"alisema Ikram.


Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa, aliwataka Wanafunzi  hao kusoma kwa bidii  na kujiepusha na vishawishi  vinavyoweza kukatisha ndoto zao  kwani serikali kwa kushirikiana  naye wameweza kuweka mazingira  bora ya kujifunzia na wamepeleka walimu wa kutosha ambapo shule hiyo iliyogharimu kiasi cha sh. milioni 470 .


" Tumejenga shule hii kwa kushirikiana na wananchi ambapo tulianza kujenga kwa nguvu za wananchi madarasa manne na baadaye tumeongeza sita kwa fedha za Serikali, wazazi wamejitolea sana na wameitikia wito niwaombe wawasimamie wanafunzi wasome kwa bidii hadi wafike chuo kikuu  kwani elimu ndio msingi  wa maisha tunawaandaa vijana Kuja kusaidia taifa hili",alisema Kawawa


Makamu mkuu wa shule ya Sekondari Msisima  alisema shule hiyo imekuwa mkombozi kwa wanafunzi hao ambapo wanafunzi hawa walikuwa wakifauhulu 30 hadi 34 kwenda kuendele kidato cha kwanza lakini kutokana na umbali wanafunzi waliokua wakimaliza ni wanafunzi watatu au wanne tu.


Alisema ,Shule  inakadiriwa kuchukua wanafunzi wapatao 400 ambapo kwa sasa kuna idadi ya wanafunzi 134  kidato cha tatu wapo 19, kidato cha pili wapo 42 na kidato cha kwanza wapo 73, shule hii ina idadi ya walimu 9 akiwemo Mwalimu  wa kike mmoja na Walimu wa kiume wapo 8.


Naye Fatma Ally makazi wa Matapwende alisema amefurahishwa na jitihada  za kuleta maendeleo ambazo zimefanywa na Mbunge kwa kuweza kusimamia ujenzi wa shule za sekondari  kwa kushirikiana na wananchi wake na kuyamalizia.


Mwisho.

No comments: