Mfanyabiashara maarufu Tanga adaiwa kupotea - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 24 July 2024

Mfanyabiashara maarufu Tanga adaiwa kupotea





NA: Burhani Yakub,Tanga.


maipacarusha20@gmail.com 


Wakazi wa mtaa wa Kange Mjimwema wamekumbwa na taharuki baada ya mfanyabiashara maarufu ambaye ni jirani yao kupotea katika mazingira ya kutatanisha.


Mfanyabiashara huyo,Enock Chambala (41) pichani ambaye ni mmiliki wa kampuni ya kununua,kuchakata na kuuza nchi za nje Mkonge hajulikani alipo kwa siku 18 hadi leo jumatano asubuhi.


Taarifa za kupotea kwa mfanyabiashara huyo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga Almachius Mchunguzi na kwamba jeshi hilo linachunguza tukio hilo.


Bernad Mapunda ambaye ni jirani wa mfanyabiashara huyo amesema tangu Julai 6 mwaka huu hakuonekana na hajulikani alipo.


"Chambala ni jirani yetu tangu Julai 6 mwaka huu hatujamuona tukapata wasiwasi na kuanza kufuatilia aliko lakini leo ni siku ya 18 hapatikani kwenye simu wala hatujui yuko wapi...hili tukio limetupa taharuki kubwa jirani zake"alisema Mapunda.


Msaidizi wa mfanyabiashara huyo,Amduni Abdallah (33) amesema aliachana naye Julai 6 mwaka huu saa 1.00 jioni baada ya kufunga ofisi lakini walishangaa kesho yake hakufika ofisini na hata kwenye simu yake hakupatikana.


"Mimi na wenzangu tuliachana na bosi saa 1.00 jioni alituaga kuwa anakimbilia nyumbani na kwa sababu si mnywaji wa pombe mara nyingi akitoka kazini huenda nyumbani kwake Kange Mjimwema"amesema Amduni.


Baraka Chambala ambaye ni mdogo wake mfanyabiashara huyo amesema amelazimika kuwasili Tanga akitokea Ngara mkoani Kagera kwa ajili ya kumtafuta kaka yake lakini kutokana na siku kusonga mbele bila kuonekana anakata tamaa ya kumpata.


Baraka ambaye ni afisa masoko wa Redio Kwizera amesema taarifa za kupotea kwa kaka yake zimetolewa katika ngazi mbalimbali ikiwamo kwa Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa,Afisa Mtendaji wa mtaa wa Kange Mjimwema,Diwani wa Kata ya Maweni Joseph Korvas,Mkuu wa Wilaya ya Tanga kituo cha polisi Chumbageni Tanga na hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo kutafuta kama amelazwa au mwili wake upo mochwari.


"Jalada la uchunguzi lilifunguliwa kituo cha polisi Chumbageni jumanne jioni wiki hii..ni matumaini yetu kuwa tutapata taarifa za wapi alipo kaka yangu"amesema Baraka.


Watu waliozungumza kuhusiana na tukio hilo waliomba vyombo vya dola kuingilia kati kwa kichunguza kama Kuna genge maalumu linaloendesha vitendo vya utekaji wa wananchi hatimaye vikome ili kuondoa wasiwasi na taharuki iliyojitokeza katika kipindi hiki.


"Tunashindwa hata cha kufanya,kila kukicha tunasikia huyu katekwa,mara huyu kapotea katika mazingira ya kutatanisha...tunaomba vyombo vya dola viingile kati ili kuirejesha Tanga katika utulivu na amani yake ya asili"amesema Doto Hussein.


Diwani wa Kata ya Maweni, Joseph Korvas amesema tukio kama hilo halijawahi kutokea katika eneo lake na kwamba amewasiliana na uongozi wa Serikali ngazi ya Wilaya na Mkoa ambao umenipa ushirikiano mkubwa katika kichunguza.

MWISHO

No comments: