MRADI WA RUWASA WA DAMBIA HAYDOM KUNUFAISHA WATU 133, 737 MANYARA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 13 July 2024

MRADI WA RUWASA WA DAMBIA HAYDOM KUNUFAISHA WATU 133, 737 MANYARA

 





Na Mwandishi wetu, Dongobesh


maipacarusha20@gmail.com 


Wananchi 133,737 wa vijiji 21 wa halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara watanufaika na huduma ya maji safi na salama kupitia mradi wa Dambia Haydom.


Meneja wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Mbulu, mhandisi Onesmo Mwakasege amesema mradi huo utawanufaisha watu 133,737 wa vijiji 21.


Mwakasege amevitaja vijiji hivyo kuwa ni Yaeda kati, Dirim, Endalat, Endamilay, Murkuchida, Endanachan, Basonyagwe na Basoderer.


Amevitaja vijiji vingine kuwa ni Bashay, Dongobesh, Qandach, Ng'wandakw, Haydom, Garbabi, Yaeda Chini, Mongo wa Mono, Domanga, Eshkesh, Endagulda na Harar.


Amesema faida ya mradi huo ni upatikanaji wa huduma ya maji karibu kwa wananchi na taasisi za umma na ajira za watu 145 zimetolewa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za ujenzi zinazoendelea.


"Gharama za ujenzi wa mradi huu ni Sh41.2 bilioni na unajengwa na mkandarasi Kings building wa jijini Dar es salaam na amepatiwa malipo ya awali Sh4.5 bilioni," amesema Mwakasege.


Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2024, Geofrey Mnzava amewapongeza RUWASA kwa namna wanavyosimamia mradi huo.


"Mwenge wa uhuru umeridhia kuweka jiwe la msingi mradi wa maji wa Dambia Haydom, tunatarajia mradi utakamilika kwa wakati ili jamii inufaike," amesema Mnzava.


Amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha kwa ajili ya kufanikisha mradi huo hivyo wananchi wana matarajio makubwa ya kupata maji.


Mkazi wa kijiji cha Arsha,  Pascal Raphael amesema mradi huo pindi ukikamilika utanufaisha jamii ya eneo hilo.


Raphael amesema awali walikuwa wanatoa maji mtoni ambayo yalikuwa machafu kwani wakulima wa zao la vitunguu swaumu walikuwa wanamwagia mabaki ya dawa za viuatilifu.


"Pia tulikuwa tunapata magonjwa ya homa ya matumbo sababu ya maji hayo ila mradi huu wa Dambia Haydom utakuwa faraja kwetu," amesema.

No comments: