NABERERA WAKUSANYA MILIONI 51 UJENZI NYUMBA YA WALIMU SOITO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 25 July 2024

NABERERA WAKUSANYA MILIONI 51 UJENZI NYUMBA YA WALIMU SOITO

 


Na Mwandishi wetu, Simanjiro 


maipacarusha20@gmail.com 


WAKAZI wa Kata ya Naberera Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wadau wa maendeleo na viongozi mbalimbali wamefanikisha kukusanya shilingi milioni 51 za ujenzi wa nyumba ya walimu kwenye shule shikizi ya Soito.


Wananchi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Naberera Richard Kusumba wamefanya harambee hiyo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili kwa moja ya walimu watakaokuwa wanawafundisha wanafunzi hao ambapo lengo lilikuwa kupata shilingi milioni 65.


Katibu Tawala (DAS) wa wilaya ya Simanjiro, Warda Abeid akizungumza kwa niaba ya DC Simanjiro Fakii Raphael Lulandala baada ya kuzindua madarasa hayo amesema harambee hiyo imefanikisha Sh51.8 milioni za ujenzi wa nyumba mbili kwa moja ya walimu.


Warda amewapongeza wote walioshiriki harambee hiyo na kupatikana kiasi hicho japokuwa lengo lilikuwa kukusanya kiasi cha Sh65 milioni.


"Kazi kubwa imefanyika nawapongeza mno hasa Mwenyekiti Mwenyekiti wa kijiji Richard Kusumba ila fedha hizo zitumike kwa lengo lililokusudiwa ili nyumba hiyo iweze kujengwa na kukamilika," amesema Warda.


Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amempongeza Mwenyekiti wa kijiji cha Naberera Richard Kusumba kwani ni miongoni mwa wenyeviti wanne wanaoongoza Simanjiro kwa kufanikisha miradi ya maendeleo.


"Sifanyi kampeni kwa mtu ila Mwenyekiti wa kijiji Kusumba amefanya kazi kubwa mno kwenye miradi ya maendeleo hasa ya elimu hivyo anapaswa kupewa kipindi kingine tena, " amesema Ole Sendeka 


Hata hivyo, ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia kata ya Naberera Sh2.5 bilioni za miradi ya maendeleo.


Mwenyekiti wa kijiji cha Naberera, Richard Kusumba amesema kati ya vitongoji saba, vitongoji vitano hivi sasa vina shule hivyo watoto hawataenda umbali mrefu kufuata elimu ila bado vitongoji viwili.


Kusumba amesema baada ya kuona watoto wadogo wanatembea umbali mrefu kwenda shule, alishirikiana na wakazi wa vitongoji hivyo ili kufanikisha ujenzi wa shule hizo.


"Nawashukuru wote mlioshiriki harambee hii kwa wale niliowaalika na wale ambao hawakupata mualiko ila mmeshiriki nasi kuchangia fedha za ujenzi wa nyumba ya walimu," amesema Kusumba.


Diwani wa kata ya, Naberera, Marco Munga amesema ujenzi wa shule hiyo pamoja na kurahisisha ukaribu wa elimu pia inawapndolea hofu watoto ya kukutana na wanyama wakali njiani.


"Mtoto akitembea umbali wa kilomita 12 kwenda shule anakuwa amechoka hivyo umwambie arudi tena nyumbani kilomita 12 anapata hofu,"  amesema Munga.


Ofisa mtendaji wa kijiji cha Naberera, Mary Moria, akizungumza baada ya kuzinduliwa madarasa matatu ya shule shikizi ya Soito amesema hivi sasa bado vitongoji vya Engutoto na Naibor- Enderit hazina shule.


Moria amesema ujenzi wa madarasa matatu ya shule hiyo umegharimu Sh27.2 milioni na hivyo kufikisha shule nne zilizojengwa hivi karibuni kwenye vitongoji tofauti.


Mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo ya Soito, James Samweli amewashukuru wazazi na walezi wa eneo hilo kwa kuwajengea shule eneo la karibu na makazi kwani watasoma kwa raha na kutotembelea umbali mrefu.


MWISHO

No comments: