OLENGURUMWA ASHINDA PINGAMIZI LA KESI INAYOPINGA WATU KUSHTAKIWA KWENYE MAHAKAMA ZISIZO NA MAMLAKA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 30 July 2024

OLENGURUMWA ASHINDA PINGAMIZI LA KESI INAYOPINGA WATU KUSHTAKIWA KWENYE MAHAKAMA ZISIZO NA MAMLAKA

 

Wakili Onesmo Olengurumwa ambaye pia ni Mratibu wa mtandao wa watetezi wa haki za Binadamu Tanzania 


Na Mwandishi Wetu 


maipacarusha20@gmail.com


Mahakama ya Rufaa ya Tanzania jijini Dar es Salaam imetoa uamuzi kuhusu rufaa iliyokuwa inapinga vifungu vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambavyo vinaruhusu watu kushtakiwa kwenye Mahakama ambazo hazina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo. 


Akisoma uamuzi wa rufaa hiyo naibu msajili wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Kingwele amesema kwamba jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu walikosea wao kama wao kumpangia jaji mmoja kati yao kusikiliza pingamizi lililopelekea kesi ya Onesmo kutupiliwa mbali. Mahakama ya Rufaa imeamua kwamba utaratibu sahihi ni kwamba endapo kuna pingamizi limewasilishwa Mahakamani, Jaji Kiongozi au Jaji Mfawidhi ndiye anapaswa kupanga jaji wa kusikiliza pingamizi hilo na sio majaji wenyewe watatu kuamua nani wa kusikiliza kati yao. 



Mahakama ya Rufaa kupitia uamuzi wake huo wa leo imeelekeza kesi hiyo irudi tena Mahakama Kuu kwaajili ya kupangiwa Jaji wa kusikiliza pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2019 kuwa kesi hiyo inafanana na kesi iliyowahi kuamuliwa miaka ya nyuma (kesi ya Galeba)



Kesi hiyo ilisikilizwa Julai 09, 2024 mbele ya jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa ambao ni Mhe. Jaji Mlacha, Mhe. Jaji Mwarija na Mhe. Jaji Rumanyika. 


Kesi hiyo ilifunguliwa na Mtetezi mahiri wa Haki za Binadamu, Wakili Onesmo Olengurumwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2021 na ilisikilizwa tarehe 09.07.2024 katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania, jijini Dar es Salaam mbele ya jopo la Majaji watatu, Mhe. Jaji Rumanyika, Jaji Mwarija na Jaji Mlacha. 


Rufaa hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania masijala ya Dar es Salaam uliotolewa mwaka 2020 ambapo Mahakama kuu ilitupilia mbali kesi hiyo kwa misingi ya kwamba aina ya maombi na  kiini cha msingi katika maombi hayo, tayari ilikwisha amriwa katika mashauri ya awali (Res Judicata)


kesi hiyo ilikuwa inapinga vifungu vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai vinavyoruhusu washtakiwa kushtakiwa kwenye mahakama za chini ambazo hazina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo (committal Proceedings). 


Vifungu vilivyolalamikiwa ni namba 178, 243, 244, 245, 246, 247, 248, 249, 250, 256, 257,258 na 259 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kwa minajili ya kuwa vinakiuka Katiba na haki za binadamu kwa mfano haki ya kusikilizwa kwa usawa, usawa mbele ya sheria n.k. ambazo zipo katika Ibara ya 13 (1) (2) na (6) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.


Hoja za Rufaa zilikuwa mbili ambazo  ni: 


 Mahakama Kuu ilikosea kutupilia mbali kesi hiyo kwa kigezo kuwa kiini na aina ya kesi hiyo ilikwisha amriwa katika kesi ya Galeba. Kwasababu kesi ya Galeba ilipinga vifungu viwili tu, wakati kesi ya Olengurumwa inapinga vifungu 13 vya CPA. 


 ⁠Kwamba jopo la majaji wa Mahakama Kuu walikosea wao kama wao kumpangia Jaji mmoja kati yao ili kusikiliza pingamizi lililopelekea kesi hiyo kutupwa kinyume na utaratibu ambapo ilitakiwa Jaji Kiongozi ndiye apange Jaji mmoja kwaajili ya kusikiliza pingamizi.


 Baadhi ya WANANCHI wakizungumzia maammuzi haya ,waliitaka Serikali kuanza kutekeleza ili Kulinda haki za watu badala ya kufikiria kupinga Tena.

Julius Minja mkazi wa Arusha alisema WANANCHI wengi wamekuwa wakipata shida kutokana na kesi zao kukaa muda mrefu bila kusikikizwa kwenye MAHAKAMA ambazo hazina MAMLAKA.


"Binafsi napongeza maamuzi haya na ninampongeza ole ngulumwa kwa kufungua kesi hii kwani inakwenda Kulinda haki za Binadamu "alisema


Sara leshaine mkazi wa Monduli alitaka jeshi la Polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka kuona kesi hiyo Ina manufaa kwao kwani inakwenda kupunguza malalamiko ya muda mrefu ya kesi kukaa muda mrefu.


"Binafsi sioni shida katika hii kesi wahusika wangekubali tu kwenda kufanya maboresho ya kanuni zao ili kesi zipelekwe mahakama husika badala ya Sasa kesi kama ya mauwaji inaanzia mahakama za chini mwaka mzima ndipo uende MAHAKAMA ya juu"alisema

No comments: