SIMANJIRO YAIBUKA NA CLEAN SHEAT NA BLUE TICK KWENYE MWENGE WA UHURU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 19 July 2024

SIMANJIRO YAIBUKA NA CLEAN SHEAT NA BLUE TICK KWENYE MWENGE WA UHURU

 



Na Mwandishi wetu, Simanjiro 

 

maipacarusha20@gmail.com 


MWENGE wa uhuru umeridhia miradi yote tisa iliyotembelea Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, yenye thamani ya shilingi bilioni 6.5 baada ya kukimbizwa kilomita 177.4.


Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, mwalimu Fakii Raphael Lulandala, akizungumza baada ya kuhitimisha mbio hizo na kukabidhi kwa mkuu wa mkoa huo Quuen Cuthbert Sendiga amesema mwenge umeridhia miradi yote tisa.


Lulandala amesema mwenge umeridhia miradi hiyo kwa kuona miradi mitano, kuweka jiwe la msingi miradi mitatu na kuzindua mradi mmoja kwenye tarafa mbili za Naberera na Moipo.


Ametaja miradi hiyo ni kutembelea mradi wa kitalu nyumba wenye thamani ya shilingi milioni 87 uliopo kata ya Orkesumet na kutembelea mradi wa mwaka jana wa ujenzi wa barabara ya lami mji mdogo wa Orkesumet, wa thamani ya shilingi milioni 665.   


“Mwenge umetembelea na kuona mradi wa Mirerani Youth garden wenye thamani ya shilingi milioni 7 na kuzindua madarasa mawili na matundu ya choo shule ya sekondari Mirerani B.W. Mkapa wa thamani ya shilingi milioni 2” amesema Lulandala.


Amesema mwenge wa uhuru umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji Mirerani wa thamani ya shilingi bilioni 4.373 na kuweka jiwe la msingi kituo cha afya Tanzanite cha thamani ya shilingi milioni 500.


Amesema mwenge umeweka jiwe la msingi barabara ya lami ya kilomita 1.2 ya sokoni hadi lango la kuingia migodi ya Tanzanite Mirerani ya thamani ya shilingi milioni 949.


"Pia mwenge umetembelea kituo cha kulelea watoto wenye uhitaji maalum cha Light In Africa na kukagua mabanda yaliyopo kwenye uwanja wa barafu wa CCM kata ya Endiamtu," amesema.


Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka huu wa 2024 Godfrey Mzava ameipongeza Simanjiro kwa namna walivyoutendea haki mwenge wa uhuru.


"Tunawapongeza Simanjiro kwani mwenge umekimbizwa na tumepata ushirikiano kwa viongozi na jamii kwa ujumla kwa kila mahali mwenge ulipopita," amesema Mzava.


Hata hivyo, amempongeza mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka kwa kushiriki kuanzia mwanzo hadi mwisho katika kukimbiza mwenge wa uhuru kwenye eneo hilo.


"Tumeona hamasa kubwa kwenye nyimbo na kuwapa moyo wakimbiza mwenge wa uhuru kitaifa, Ole Sendeka anastahili pongezi kwenye hilo," amesema Mzava.


Ujumbe mahususi wa mwenge wa uhuru kwa mwaka 2024 ni Tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu.



MWISHO

No comments: