MWENGE WAZINDUA MRADI WA MAJI BWAGAMOYO KIBAYA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 19 July 2024

MWENGE WAZINDUA MRADI WA MAJI BWAGAMOYO KIBAYA

 




Na Mwandishi wetu, Kiteto 


maipacarusha20@gmail.com 


MWENGE wa uhuru umezindua mradi wa maji wa Bwagamoyo Kibaya Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, utakaonufaisha watu 2,960.


Meneja wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilayani Kiteto, mhandisi Stephano Mbaruku akizungumza wakati mwenge wa uhuru ukizindua mradi huo amesema umegharimu shilingi 422,034,447.30.


Mhandisi Mbaruku amesema chanzo cha maji ni kisima kirefu cha mita 100 chenye uwezo wa kuzalisha lita 18,000.


Amesema chanzo fedha za mradi huo ni program ya P for R na mkandarasi ni kampuni ya M/S Juin company limited.


Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji Kibaya (KIUWASA) Charles Mpondo akisoma taarifa ya mradi huo amesema tangi la maji lina lita 300,000


Mpondo amesema mradi una tangi la kuongeza msukumo wa maji lenye ujazo wa lita 25,000 juu ya ardhi, vituo tisa vya maji, chemba 22 na mtandao wa bomba wa kusambaza maji urefu wa mita 11,010.


Amesema chanzo cha maji ni kisima kirefu cha mita 100 chenye uwezo wa kuzalisha lita 18,000 kwa saa.


Mbunge wa Jimbo la Kiteto Wakili msomi, Edward Ole Lekaita Kisau amewapongeza RUWASA kwa kukamilisha mradi huo ambao una manufaa makubwa kwa jamii.


"Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kutupa fedha zilizokamilisha mradi huu utakaoongeza chachu ya maendeleo kupitia sekta ya maji," amesema Ole Lekaita.


Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2024, Geofrey Mzava pamoja na kuwapongeza RUWASA kwa kufanikisha mradi huo ameitaka jamii ya eneo hilo kuutunza.


"Maji ni uhai, hakikisheni mnautunza mradi huu kwa manufaa yenu na kizazi kijacho kwani serikali imeshatekeleza wajibu wake kwa kufanya hili nanyi timizeni kwa kufanya yenu," amesema Mzava.


Mkazi wa kijiji cha Bwagamoyo, Malami Laizer ameipongeza RUWASA kwa kukamilika mradi huo ambao utawasaidia wananchi wa eneo hilo kwani miaka iliyopita walikuwa wanatumia maji yasiyo masafi.


Laizer amesema maji hayo hayana chumvi wala ubaya na watakuwa wanalinda mradi na mazigira yake.


Mkazi mwingine Loishiye Mollel amesema waliteseka kwa muda mrefu kwani baadhi ya watu walipata maradhi ya tumbo kwa kunywa maji ya korongoni.


"Tunawashukuru RUWASA kwa mradi huu kwani kule korongoni kuna watu walikuwa wanajisaidia haja kubwa sasa wengine waliokuwa wanakunywa maji ya hayo na kusababisha maradhi ya tumbo," amesema.


MWISHO

No comments: