WAZIRI KAIRUKI AITAKA TAWA KUTUMIA MIRADI YA UJIRANI MWEMA KUTATUA CHANGAMOTO, AITAKA KUENDELEA KUSIMAMIZI RASILIMALI ZA WANYAMAPORI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 9 July 2024

WAZIRI KAIRUKI AITAKA TAWA KUTUMIA MIRADI YA UJIRANI MWEMA KUTATUA CHANGAMOTO, AITAKA KUENDELEA KUSIMAMIZI RASILIMALI ZA WANYAMAPORI

 






Na: Lilian Kasenene,Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuendeleza usimamizi wa rasilimali za wanyamapori huku akitaka miradi ya ujirani mwema ijikite katika kutatua changamoto kama vile ujengaji wa vizimba.


Kairuki alisema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika ofisi za Makao Makuu ya TAWA yaliyopo Mkoani Morogoro kwa lengo la kusikiliza changamoto na kutoa utatuzi ili kuboresha utendaji kazi wa TAWA.


"TAWA Kuweni na usimamizi mzuri wa rasilimali ya wanyamapori kwa kuzingatia kuwa ni Taasisi ambayo haina muda mrefu tangu kuanzishwa kwake, na tatueni changamoto zilizopo," alisema


Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki alipata wasaa wa kuzungumza na watumishi wa TAWA ambapo alisisitiza kuhusu uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Miongozo na taratibu katika kutimiza majukumu yao ili kuboresha utendaji kazi.


Akizungumza kuhusu changamoto ya wanyama wakali na waharibifu iliyowasilishwa na Menejimenti, Kairuki alielekeza kuwa miradi ya ujirani mwema ijikite katika kutatua changamoto hiyo kama vile ujengaji wa vizimba pamoja na utoaji wa vitendea kazi kama pikipiki ili kuweza kupunguza changamoto hiyo.


Kamishna wa Uhifadhi -TAWA, Mabula Misungwi Nyanda akizungumza katika ziara hiyo aliaihidi kuendeleza usimamizi katika taasisi hiyo na kutekeleza maagizo na maelekezo yaliyotolewa na Waziri Kairuki baada ya kuitembelea TAWA.


Naye Kaimu Naibu Kamishna anayeshughulikia huduma za uhifadhi, Mlage Kabange alitoa taarifa kuhusu maeneo yanayosimamiwa na TAWA, mafanikio na jitihada zinazofanywa na katika kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo wamekuwa wakinunua vifaa na kuvitoa kwa jamii zinzozunguka hifadhi ama mapori ya akiba.


Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Fortunata Msoffe, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii, Abdallah Mvungi pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Wizara ya Maliasili na Utalii, Lucy Saleko.



No comments: