AUWSA KUTUMIA BILIONI 8.3 KUFIKISHA MAJI MACHIMBO YA TANZANITE MERERANI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 5 August 2024

AUWSA KUTUMIA BILIONI 8.3 KUFIKISHA MAJI MACHIMBO YA TANZANITE MERERANI

 


Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira jiji la Arusha, Justin Rujomba (katikati) akielezea mipango ya kufikisha maji kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite katika kikao cha eneo tengefu la Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, kulia ni Ofisa madini mkazi Mirerani, Nchagwa Marwa Chacha.


Na Mwandishi wetu, Mirerani


maipacarusha20@gmail.com 


WACHIMBAJI wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wanatarajia kunufaika na mradi wa maji baada ya Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira jiji la Arusha, (AUWSA) wenye thamani ya Sh8.3 bilioni.


Mkurugenzi mtendaji wa AUWSA, Justin Rujomba ameyasema hayo wakati akizugumza na waandishi wa habari juu ya mikakati ya kuwapatia maji safi na salama wachimbaji madini ya Tanzanite Mirerani.


Rujomba amesema baada ya kupatikana fedha hizo Sh8.3 bilioni wataanza kuweka miundombinu ya maji kwani wameshafanya utafiti kupitia wataalam kisha kusambaza maji.


Amesema hivi sasa wamejipanga kutekeleza agizo la mkuu wa wilaya ya Simanjiro Fakii Lulandala la kufikisha huduma ya maji kwa wachimbaji madini ya Tanzanite ndani ya siku saba.


Amesema watafanikisha hayo kupitia mipango miwili ambapo mpango wa muda mfupi watatekeleza kwa kutumia magari kisha mpango wa muda mrefu watasambaza maji ya bomba.


“Kwenye mpango wa muda mrefu tunatarajia kutumia Sh8.3 bilioni na itakuwa suluhisho ya kupatikana kwa maji safi na salama kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite,” amesema Rujomba.


Amesema kwenye mpango wa muda mfupi wataingiza maji kupitia magari yatakayokuwa yamebeba maboza ya lita elfu 10 wakitumia bei elekezi ya serikali ambayo imepangwa na (EWURA).


“Magari yatakuwa yanachota maji safi na salama yaliyopo mji mdogo wa Mirerani na kuyaingiza ndani ya ukuta unaozunguka madini ya Tanzanite kwa kuyamwaga kwenye matenki yaliyopo ndani,” amesema.


Amesema baada ya hapo watatimiza mpango wa muda mrefu wa kufikisha maji kwani wameshafanya utafiti na kusubiria fedha hizo Sh8.3 bilioni ambazo zitafanikisha miundombinu ya maji.


Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala amesema ametoa muda wa siku saba kwa AUWSA kuhakisha wachimbaji na watu waliopo ndani ya ukuta wanapata maji.


“Tumewaagiza AUWASA wasambaze maji ndani ya siku saba na baadaye wahakikishe wanafanikisha upatikanaji wa maji safi na salama kupitia boma,” amesema Lulandala.


Mmoja kati ya wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite, Bahati Mushi amesema hatua ya upatikanaji maji kwenye eneo hilo itakuwa maendeleo makubwa kwani maji ni uhai.


“Wachimbaji tukipata maji itakuwa vyema mno na tunampongeza Waziri wa Maji Jumaa Aweso ambaye anafanya kazi kubwa kuhakikisha watu wa maeneo mbalimbali wanapata maji,” amesema Mushi.


MWISHO

No comments: