BIOANUAI 3,935 ZABAINIKA KWENYE HIFADHI TATU ZA MISITU YA ASILI SAFU ZA MILIMA YA TAO LA MASHARIKI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 30 August 2024

BIOANUAI 3,935 ZABAINIKA KWENYE HIFADHI TATU ZA MISITU YA ASILI SAFU ZA MILIMA YA TAO LA MASHARIKI

 





Na Lilian Kasenene,Morogoro.

maipacarusha20@gmail.com


WATAFITI kutoka chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) kupitia mradi wa Utafiti wa kuongeza matumizi ya taarifa za bioanuai kwa uhifadhi endelevu na kipato kwenye Milima ya Tao la mashariki nchini Tanzania wabaini uwepo wa zaidi ya Bioanuai 3,935 kwenye hifadhi tatu za Misitu ya asili.


Hifadhi hizo za MISITU ya asili ni Kilombero, Uzungwa na Uluguru zilizopo mkoani Morogoro.


Mkuu wa mradi huo wa utafiti Profesa Pantaleo Munishi kutoka Idara ya Mifumo Ikolojia na Uhifadhi katika SUA alitoa takwimu hizo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa maafisa uhifadhi kutoka kwenye misitu hiyo mitatu ya asili ya hifadhi iliyo kwenye Safu za milima ya Tao la mashariki.



Alisema matokeo hayo ya utafiti yatasaidia wahifadhi kutambua na kuweka mikakati ya namna ya kutunza bioanuai hizo na kuzitangaza ulimwenguni ili kuongeza tija.


“Milima ya Tao la mashariki ni moja ya maeneo muhimu ya Bioanuai  yanayotambulika kidunia na kupewa kipaumbele ili kutunzwa na kumekuwapo kwa miradi mingi ya utunzaji wa misitu na Bioanuai zilizomo lakini kumekuwa hakuna taarifa sahihi za Bioanuai zilizomo katika kipindi chote cha utekelezaji wa miradi hiyo” alifafanua Prof. Munishi.


Aidha alisema kuwa taarifa zilizopo pia hazipo sehemu moja kiasi cha kuwa rahisi wahitaji kuzipata kirahisi hivyo kuchangia kupunguza jitihada za kuzitangaza lakini pia kuzihifadhi hasa katika kipindi hiki mabacho mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa makubwa na kupelekea kuathiri bioanuai nyingi na zingie kupotea.


Mtafiti huyo mkuu alisema baada ya kukamilisha utafiti wao wa kuzitambua bioanui zinazopatikana kwenye misitu hiyo mitatu ya hifadhi ya asili iliyo kwenye milima ya tao la mashariki wameamua kuwaita maafisa uhifadhi kutoka misitu hiyo na kuwapatia lakini pia kuwafundisha namna bora za kutumia mifumo ya kimtandao kuzitangaza ili zifahamike duniani kote na kutunzwa.


Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Misitu na nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk Ezekiel Mwakalukwa alisema kuwa matokeo mazuri ya utafiti yakitunzwa vizuri katika sehemu moja na kuwezesha kupatikana kirahisi yanaweza kusaidia jamii na Serikali kufanya maamuzi sahihi ambayo yataleta tija kwa Wananchi na Taifa.


“Bioanuai ni rasilimali muhimu sana kwa maendeleo ya jamii na taifa na mara nyingi kutokuwa na taarifa zake sahihi katika nchi au misitu kunapelekea uhifadhi wake kuwa mgumu na zingine kutoweka hivyo tafiti zinasaidia sana kuzitambua lakini kuweka mipango madhubuti ya kuzihifadhi ili ziendelee kutoa mchango stahiki kwenye maendeleo” alieleza Dk Mwakalukwa. 


Aliongeza “Nipongeze kazi kubwa iliyofanywa na Mradi huu unaaongozwa na Prof. Pantaleo Munishi kutoka hapa SUA kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kufanya utafiti katika misitu yetu mitatu ya hifadhi ya asili iliyo kwenye milima ya Tao la mashariki kubainisha bioanuai muhimu zilimo na kuwezesha taarifa zake kupatikana na hivyo kuwa rahisi kuzitangaza dunaini na kusaidia mipango ya serikali na wasimamizi wa misitu hiyo kupanga mipango bora ya kuzihifadhi”.


Nae Alan Kimbita ambaye ni afisa mipango na mawasiliano kutoka Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF) ambao ndio wafadhili wa mradi huo wa utafiti wamepongeza kazi iliyofanywa na watafiti hao kutoka SUA na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kuja na taarifa hizo muhimu na hivyo kuwezesha kutambua Bioanuai zilizopo kwenye maeneo hayo kwa sasa.


“Baada tu ya kuchapisha baadhi ya viumbe hai waliobainika kwenye misitu hiyo tayari tumeanza kupata maswali kutoka maeneo mbalimbali duniani wakitaka kujua vinapopatikana na hii ni ishara njema kuwa kama taarifa zote zitakusanywa hivi na kutangazwa kikamilifu zitavutia wadau wengi sana kuja kuzitembelea kuziona na wengine kufanya tafiti na kusaidia uhifadhi” alisema Kimbita.


Utafiti huo ulibainisha bioanuai za Mimea, Ndege, Wanyama, Mijusi na vingine na kupitia mafunzo hayo wataweza kuweka mikakti ya kuhakikisha vinatangazwa kwenye mitandao yote na kuwekwa kwenye mfumo wa taarifa za bioanuai za Tanzania (TanBIF) na ule wa dunia yaani (BGIF).

No comments: