DIWANI TAIKO ASIMIKWA KUWA LAIGWANANI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 11 August 2024

DIWANI TAIKO ASIMIKWA KUWA LAIGWANANI

 



Na Mwandishi wetu, Simanjiro 


maipacarusha20@gmail.com


DIWANI wa Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Taiko Kurian Laizer amesimikwa kuwa kiongozi wa kimila wa jamii ya kifugaji (Laigwanani)


Taiko amesimikwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Manyara, Peter Toima ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye shughuli hiyo iliyohudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.


Taiko akizungumza baada ya kusimikwa kuwa kiongozi wa kimila ameahidi kutumia nafasi hiyo kwa kutenda haki bila kumuonea mtu yeyote.


"Nawashukuru watu wote waliohudhuria sherehe hii, ndugu zangu na wake zangu kwa kunipa joto kwenye kusimikwa kwangu kuwa kiongozi wa kimila," amesema Taiko.


Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara, Peter Toima amempongeza Taiko kuwa kiongozi wa kimila hivyo aendelee kuwatumikia watu kwa uadilifu, imani na upendo.


Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Manyara, amewaasa wakazi wa eneo hilo kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na kuchagua wagombea kupitia chama hicho.


Mbunge wa jimbo la Kiteto Wakili msomi Edward Ole Lekaita Kisau amempongeza Taiko kwa kusimikwa kuwa kiongozi wa kimila huku akiendelea kutumikia jamii yake kwa nafasi ya udiwani.


"Pamoja na salamu kutoka kwa majirani zenu wa Kiteto, tunaendelea kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna kila sehemu inavyopatiwa miradi mbalimbali ya maendeleo," amesema Mbunge huyo.


Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amempongeza Diwani huyo wa kata ya Naisinyai Taiko kwa kusimikwa kuwa kiongozi wa kimila.


"Tunakupongeza ndiyo maana wafugaji wa Manyara, Arusha na Kilimanjaro kwa umoja wetu tumekusanyika hapa na tunaahidi kumlipia fomu ya kugombea urais mwaka 2025 mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan," amesema Ole Sendeka.


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Kiria Laizer amesema anatarajia viongozi wa kimila kusaidia katika kukemea uuzaji holela wa ardhi kwani wanaushawishi mkubwa kwa jamii.


"Wengi ni wakubwa zangu ziwafundishi kuongoza ila kupitia ninyi mtaweza kuwasimamia viongozi wa vijiji na vitongoji wasiuze ardhi au kusababisha migogoro," amesema Kiria.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga Laizer amesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa Diwani huyo ambaye ameongezewa majukumu ya kuwa kiongozi wa kimila.


MWISHO

No comments: