MIAKA 60 YA HIFADHI YA MIKUMI WAZIRI MALIASILI PINDI CHANA KUWA MGENI RASMI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 31 August 2024

MIAKA 60 YA HIFADHI YA MIKUMI WAZIRI MALIASILI PINDI CHANA KUWA MGENI RASMI

 



Kamishna wa Uhifadhi TANAPA Musa Kuji akizungumza na waandishi wa habari 

Mshindi wa kwanza wa Riadha miaka 60 ya Mikumi Shaban Sambaa akimalizia mbio


Na: Lilian Kasenene,Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


MAADHIMISHO ya miaka 60 toka kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi yametanguliwa na Michezo mbalimbali ikiwemo Riadha ambapo wakimbiaji zaidi ya hamsini wamekimbia mbio za kilometa kumi(10) ndani ya hifadhi hiyo.


Mbio hizo zilishirikisha washiriki zaidi ya 80 kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Morogoro, ambapo mshindi wa kwanza katika mchezo wa Riadha kwa upande wa wanaume alikuwa ni Shaban Sambaa mkazi wa Ruaha wilayani Kilombero aliyetumia dakika 30 na sekunde 20.


Mshindi kwanza kwa wanawake ni Pili Samuel aliyeshika nafasi ya saba kwa washiriki wote aliyetumia dakika 40 akitokea hifadhi ya Taifa ya Udzungwa.


Kwa wanaume mshindi wa pili ni Kangala Shija aliyetokea jijini Mwanza ambaye alikimbia dakika 36 na sekunde 4,huku mshindi wa tatu Venance Mtungi akikimbia dakika 36 na sekunde 56.


Akizungumza baada ya kukamilika kwa mbio hizo ambazo wakimbiaji  walivalishwa medali na  Kamishna wa Uhifadhi, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Kuji, Kamishna huyo alisema michezo ni moja utalii hivyo kuwepo kwa Riadha na Michezo mingine hifadhini kunajenga hali na utayari wa watalii kuona umuhimu wa kuimarisha afya kwa njia hiyo.


Kamishna Kuji alisema kufanya michezo ndani ya hifadhi kunasaidia kuendelea kuzitangaza hifadhi za Taifa ikiwemo Mikumi ambayo kwa sasa imekuwa na ongezeko kubwa la watalii na mapato na kwamba ulinzi umekuwa ukiimarishwa wakati wote wa michezo.


Mshindi wa kwanza Sambaa alisema maandalizi yamekuwa mazuri na yenye ulinzi wa kutosha na rafiki kwa wakimbiaji kwani njia na huduma vilikuwa ni nzuri.


Sambaa alisema hayo sio mashindano yake ya kwanza kushiriki kwani amewahi pia  kushiriki Riadha katika mashindano mbalimbali nchini ikiwemo SELOUS ambapo alishika nafasi ya tatu na huku akidai mwaliko huo kupitia mtandaoni.


"Sikuwa na hofu hata kidogo kwani tulielezwa kabisa ulinzi dhidi ya wanyama uliimarishwa,"alisema Sambaa.


Naye mshindi wa kwanza wanawake Pili Samuel alieleza  kusikitishwa na ushiriki mdogo wa wanawake katika mbio hizo za maadhimisho ya miaka 60 ya Mikumi huku akiwataka kujitokeza na kutokata tamaa.


Katika maadhimisho hayo michezo mbalimbali imechezwa ikiwemo Mpira wa miguu kati ya VETA Mikumi na Kambi ya Jeshi ya Mikumi Riadha, Nyavu, Pete, kufukuza Kuku,kukimbia na magunia, Volleyball  na mpira wa kikapu.


Waziri wa Maliasili na Utalii balozi Dk Pindi Chana atakuwa Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya miaka 60 Mikumi.


Mwisho.

No comments: