UZINDUZI WA MRADI WA ULINZI NA UHIFADHI WA VYANZO VYA MAJI - MINDU. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 2 August 2024

UZINDUZI WA MRADI WA ULINZI NA UHIFADHI WA VYANZO VYA MAJI - MINDU.







Na Lilian Kasenene, Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com




KATIBU Tawala Mkoa wa Morogoro Dk Mussa Ali Mussa amezindua rasmi utekelezaji wa Mradi wa Uhifadhi na Ulinzi wa Bwawa la Mindu unaotekelezwa kwa ushirikiano kati Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu na Mamlaka ya MORUWASA kwa ufadhili wa World Water Worx unaogharimu zaidi ya kiasi cha Shilingi Bilioni 2.




Aidha mradi huo una mchango wa serikali na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili.




Mradi huo unalenga kulinda na kuhifadhi mazingira ya eneo la Mindu ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi za kimazingira ambapo utekelezaji wa mradi huu utahusisha hatua mbalimbali za uhifadhi na Urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa na shughuli mbalimbali za kibinaadamu hasa kilimo na ufugaji.




Akizungumza katika Hafla hiyo ya uzinduzi, Dk Mussa alisisitiza suala la ushirikishwaji wa jamii katika ulinzi wa vyanzo vya maji kwa kuwaletea miradi itakayokwenda kuondoa umasikini na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja.




Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Idara ya Rasilimali za Maji kutoka Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu Martine Kasambala aliainisha maeneo makuu manne ambayo yanaenda kufanyika kupitia mradi ikiwemo kuendeleza Kilimo Misitu, Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi Kaboni, Kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Sekta binafsi katika uhifadhi wa vyanzo vya maji pamoja na kujenga uwezo kwa jamii kwa kutoa mafunzo maalumu ya kuishi rafiki na mazingira.




Chanzo cha maji cha Bwawa la Mindu ndio tegemeo kubwa kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuwa ndio chanzi kikuu cha maji safi kwa zaidi ya asilima 75 kwa matumizi ya majumbani huku likiwa na ukubwa wa eneo takribani kilomita za mraba 303 lenye mito mikuu 5 inayolisha Bwawa hilo ambayo ni Ngerengere, Mgera,Malali,Mzinga na Lukulunge.




"Tone la maji lazima lihifadhiwe "

No comments: