Wafugaji wajengewa mazizi ya Waya kuzuia Simba na Fisi kula mifugo yao, Waadhimisha siku ya askari wa uhifadhi Duniani. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 1 August 2024

Wafugaji wajengewa mazizi ya Waya kuzuia Simba na Fisi kula mifugo yao, Waadhimisha siku ya askari wa uhifadhi Duniani.




Boma Hai lililojengwa na taasisi ya Chem Chem na kugaiwa kwa wafugaji ili kudhibiti simba kuvamia na kula mifugo



Baadhi ya asakari wa uhifadhi wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi

KATIBU Tawala Wilaya ya Babati Khalfani Malipula akizungumza na wakazi wa Kijiji Cha Ngolei mara baada ya kukabidhi maboma hai ya mifugo iliyojengwa na taasisi ya Chem chem

Msimamizi wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii ya Chem Chem, Napendaeli Wazoeli akimkabidhi Peter Martini Boma hai la mifugo
Katibu tawala wilaya ya Babati khalifan Mlipula akimvisha Medali askari wa uhifadhi 




Mwandishi wetu, Babati.

maipacarusha@gmail.com

Wafugaji wanaoishi ndani ya eneo la hifadhi ya jamii ya Wanyamapori ya Burunge (Burunge WMA) wilayani Babati, Mkoani Manyara na jirani na maeneo hayo, wamejengewa mazizi ya waya (Boma Hai) ili kuzuia wanyama wakali hasa Simba na Fisi kuvamia na kula mifugo nyakati za usiku.


Mazizi hayo, yamejengwa na Taasisi ya uhifadhi na Utalii ya Chem Chem, ambayo inafanya shughuli za uhifadhi na Utalii katika eneo hilo, lilipo kati kati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara ikiwa ni sehemu ya Mkakati wa Taasisi hiyo, kupunguza migogoro baina ya Wanyamapori na Mifugo.


Akizungumza wakati wa kukabidhi mazizi hayo, Mkuu wa Wilaya ya Babati , mkoa wa Manyara, Lazaro Twange alisema mradi wa ujenzi mazizi hayo ni utekelezaji wa maagizo ya serikali kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu.


Twange ambaye aliwakilishwa katika uzinduzi wa mazizi hayo na Katibu Tawala wa wilaya ya Babati, Khalfani Malipula alisema Kazi nzuri ya uhifadhi imefanyika na sasa kuna changamoto ya wanyamapori kula mifugo jambo ambalo limeanza kupatiwa suluhu.


Alisema uzinduzi wa Mazizi hayo, ambao umeambatana na maadhimisho ya siku ya Askari wa hifadhi duniani (Rangers Day), unatarajiwa pia kuwaondolea wananchi adha ya kulala nje kulinda mifugo yao.


Akizungumza baada ya kukabidhiwa Zizi lake, John Bagary mkazi wa kijiji cha Vilima vitatu alisema, hadi juzi Ng'ombe wake watano na mbuzi wanane walikuwa wameliwa na Simba.


"Nimekuwa nikilala nje kulinda Zizi langu la Ng'ombe na mara kwa mara Simba wamekuwa wakifika hapa usiku, lakini sasa nashukuru kujengewa Zizi lenye uzio la taa la mwanga wa jua ili kuzuia Simba kuruka na kuingia ndani"alisema


Mwananchi mwingine mkazi wa kijiji cha Ngoley, Peter Martin alishukuru Chem Chem na Serikali kuwajengea mazizi hayo, kwani sasa watakuwa wanalala kwa amani.


Msimamizi wa Miradi ya Maendeleo ya Jamii ya Chem Chem, Napendaeli Wazoeli alisema Chem Chem kwa kushirikiana na askari wanyamapori, waliona katika maadhimisho ya siku ya askari wa wanyamapori duniani, wakabidhi mazizi hayo.


Alisema kila zizi limekuwa likigharimu zaidi ya sh 2.6 milioni na hadi jana mazizi 15 tayari yalikuwa yamejengwa na Taasisi hiyo, ili kukabiliana na migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu.


Katika maadhimisho hayo, Chem chem walitoa vifaa vya kufukuza wanyama katika makazi ya watu, ikiwepo baruti, vuvuzela, pilipiki na toshi maalum za kufukuza wanyamapori.


Akizungumza katika maadhimisho na uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Burunge WMA, Erick Lilayoni alisema hifadhi hiyo, itaendelea kushirikiana na Chem Chem na wadau wengine ili kuhakikisha hifadhi inaendelea kuwa kivutio cha watalii.


Alisema wanaipongeza taasisi ya Chem Chem kwa msaada mkubwa ambao wamekuwa wakitoa katika Jumuiya hiyo lakini pia kwa wananchi wanaishi ndani ya hifadhi hiyo.


"Leo tumeona askari wote wanaolinda hifadhi hii wamepewa medali na vifaa vya kufukuza wanyamapori , sisi tunaamini huu ni mwendelezo tu Chem Chem kusaidia uhifadhi katika eneo letu"alisema.


MWISHO.
 






No comments: