WANANCHI 3982 WA MINJINGU KUNUFAIKA NA HUDUMA YA AFYA YA MAMA NA MTOTO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 2 August 2024

WANANCHI 3982 WA MINJINGU KUNUFAIKA NA HUDUMA YA AFYA YA MAMA NA MTOTO

 


Na Mwandishi Wetu, maipac 


maipacarusha20@gmail.com 


Zaidi ya Wananchi 3982 watanufaika na huduma ya afya itakayotolewa katika Zahanati ya Kijiji Cha Minjingu kata ya Nkaiti Mkoani Manyara hii imejiri  baada uzinduzi wa jengo la mama na mtoto kuongezeka katika Zahanati hiyo.


Kukamilika kwa ujenzi wa  jengo hilo  kutaongeza idadi ya akinamama wanaojifungulia katika hospitali kuepuka changamoto  ya umbali wa kutembea kilomita  5 kwenda katika kituo cha afya cha Nkaiti.


Zahanati  hiyo imejengwa na wawekezaji kutoka kiwanda cha mbolea cha Minjingu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya madini kwa gharama ya shilingi 52,500,000 ambapo ulianza mwezi Agosti mwaka 2023 na kukamilika 1/4,2024.

 

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Minjingu Elizabeth Lawi amesema kuwa  awali kituo hicho kilikuwa kinauwezo wa kuhudumia  wajawazito 2  ambapo kwa sasa kitahudumia wajawazito  6 hadi 10 kwa siku.


"Wakinamama walikuwa wanajifungulia nyumbani kwasababu jengo lilikuwa ni finyu sasa wanapaswa kuona umuhimu wa kujifungulia katika vituo vya afya ili kupunguza  Vifo vya mama na mtoto"


Amesema,pamoja na jitihada zilizofanyika katika ujenzi wa jengo hilo lakini Bado kuna baadhi ya changamoto kama Zahanati ya Kijiji ingependa kutatuliwa ikiwa ni pamoja na  kuongezewa jengo lingine na kuweka uzio wa kuzuia wanyama wakali hasa nyakati za usiku.


Akizungumza wakati wa kutia sahihi cheti Cha makabidhiano kwa jengo hilo Mkuu wa Wilaya ya Babati,Lazaro Twange amesema,jengo hilo limepunguza safari ya akinamama kutumia umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma ya kujifungulia na kwamba wawe tayari kupokea huduma hiyo.


Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha mbolea.cha  Minjingu,Mahesh Parik amesema tofauti na ajira  kiwanda kinafanya kazi ya kuhakikisha kwamba jamii,kinamama na watoto na masuala ya afya kwa ujumla yanafanyiwa kazi.


"Ukiondoa mradi huu,tunafanya huduma mbali mbali kwa jamii kama kutoa maji,umeme, barabara na kadhalika na pia tunaamini Kila tunachokifanya tunapaswa tutoe kwa jamii ili iweze kunufaika".


Akitoa takwimu za utekelezaji wa kufanikisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto Meneja Utawala na Rasilimali watu wa kiwanda hicho  Joram Massesa amesema kwa mwaka 2024 kiwanda hicho pia kimewekeza kwenye sekta ya maji katika kisima Cha Mswakini ambacho kitahududumia Wilaya 2 za Monduli na Babati kwenye vijiji 3 vya Minjingu ,Mswakili na Olasiti,ambapo inategemewa kutumia shilingi 130,000,000/ na kisima hicho  kimeshachimbwa katika hifadhi ya Tarangire.


Naye,afisa mtendaji wa Kijiji Cha Minjingu Salimu Mbonde amesema wakati wa kipindi cha masika wanawake waliokuwa wanataka kujifungua walikuwa wanatembea umbali mrefu kwaajili ya kufuata huduma hiyo katika kituo jirani Cha afya cha Nkaiti.


 Nao Elisifa Sangau mkazi wa Kijiji Cha Minjingu ameshukuru Ujenzi wa jengo hilo kwakuwa wakati wa mafuriko walikuwa wanaomba wadau watoe msaada kwa huduma nyingine huku Malta Ayubu amesema wamenufaika kwa ujenzi huo kwakuwa itasaidia kuepusha mama mjamzito kujifungulia njiani na kuomba Serikali kuwaongeza watoa huduma wa afya katika Zahanati ya Kijiji Cha Minjingu.

No comments: