Zaidi ya Wananchi 15000 Kunufaika na Mradi wa Maji Monduli - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 21 August 2024

Zaidi ya Wananchi 15000 Kunufaika na Mradi wa Maji Monduli



Mkurugenzi wa FELOCI, Yonas Masiaya Laizer akieleza Malengo ya mradi huo kwa mgeni Rasmi pamoja na wanufaika wa mradi huo

Mmoja wa wanufaika wa mradi akishukuru FELOCI kwa kuwaletea mradi huo


Na: Andrea Ngobole, maipac

maipacarusha20@gmail.com



Zaidi ya wakazi 15,000 wa kata ya Lesimingiroi wilayani Monduli mkoani Arusha watanufaika na maji safi na salama toka chanzo cha maji cha Losimingori chenye uwezo wa kuzalisha maji lita laki nne kwa siku.

Mradi huu, unatekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la Foundation For Empowering Local Community’s Initiative (FELOCI) lililopo Monduli Mkoani Arusha chini ya Mradi wa Mazingira unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia program ya miradi midogo ambayo inasimamiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Monduli mkoa wa Arusha, Isack Joseph aliyewakilishwa na Diwani  Nelson Lowassa katika ukumbi wa Vijana centre uliopo Ngiloriti wilayani Monduli mkoani Arusha, alisema adha ya kukosa maji wananchi wa kata hiyo inakwenda kupatiwa ufumbuzi.

Lowassa amesema kuwa uzinduzi wa chanzo hicho umekuja kwa wakati muafaka kwani maji ni changamoto kubwa inayowakabili wakazi wengi wa wilaya ya Monduli.

Amewasihi wakazi wa Lesimingori ambao watanufaika moja kwa moja na mradi huo kuhakikisha wanashiriki vema kutekeleza mradi huo pia kuulinda ili uwe na manufaa kwao na vizazi vijavyo.

Aidha mwenyekiti huyo aliunga mkono juhudi za utekelezaji wa mradi huo kwa kupatia Kijiji cha lesimingori shilingi million nne ili kufanikisha kukamilika kwa mradi huo.

Mkurugenzi wa FELOCI, Yonas Masiaya Laizer alisema wanashukuru Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia program ya miradi midogo ambayo inasimamiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kwa kuwapatia fedha za kutekeleza mradi huo kwa kata ya Lepurko.

Amesema mradi huo utanufaisha vijiji vya Losimingori, Makuyuni, Naiti, Mbuyuni na Lepurko ambapo kwa sasa wameanza kusambaza mabomba ya maji toka chanzo hicho na wanatarajia kwa awamu ya kwanza maji yatawafikia wakazi wa maeno hayo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha lesimingori Lazaro laizer amesema kuwa wanashukuru shirika hilo kuja na mradi huo kwani utawakwamua wakina Mama wa kjiji hicho waliokuwa wanalazimika kuamka usiku na kutembea kilomita 9 kwenda kutafuta maji safi na salama na kushindwa kusimamia shughuli zao za kiuchumi.

Afisa uhifadhi wa wanyamapori toka TAWA wanaosimamia na kuhifadhi chanzo hicho katika msitu wa lesimingori ndugu Laurence  amesema kuwa mradi huu utasaidia sana kuondoa mgogoro kati ya wanyamapori na wananchi wa vijiji hivyo waliokuwa wanavamia kwa ajili ya kunyweshaji mifugo Yao.

Naiji Mollel mkazi wa kjiji cha lesimingori amesema kuwa mradi huu utawanufaisha akina mama wa Kijiji hicho na kata hiyo kwani walikuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilomita 9 kwenda kusaka maji safi na salama.











No comments: