MAONYESHO YA SAMIA KILIMO BIASHARA EXPO 2024 MSIMU WA 3 KUFANYIKA GAIRO MOROGORO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 16 September 2024

MAONYESHO YA SAMIA KILIMO BIASHARA EXPO 2024 MSIMU WA 3 KUFANYIKA GAIRO MOROGORO

 





Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


MAONYESHO  ya Samia Kilimo Biashara Expo 2024 msimu wa tatu yanatarajiwa kufanyika Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro yakiwa na lengo la kuhamasisha uchaguzi wa Serikali za mitaa.


Mkuu wa mkoa wa Morogoro  Adam Malima alisema mkoa huo kupitia wilaya hiyo ya Gairo utaonyesha maonyesho makubwa ya Kilimo Biashara kwa kuhamasisha masuala mbalimbali yakiwemo ya stakabadhi ghalani.


Alisema  hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Maonyesho hayo ya Samia Kilimo biashara  Expo 2024.


Aidha alisema mbali na maonyesho hayo kusaidia kuhamasisha wananchi kushiriki katika chaguzi za serikali za mitaa pia Wananchi watatambua kuwa ni wajibu na haki yao ya msingi.


Aidha mkuu hiyo wa mkoa alitaja lengo lingine katika maonyesho hayo ni uelimishaji na uhamasishaji kuhusu ushiriki wa mfumo wa stakabadhi za ghala ambayo yatasaidia wakulima kuhifadhi mazao yao kwa usalama.


"Niwaeleze pia Mfumo huu unasaidia wakulima kuepuka kunyonywa na madalali wa mazao ambao wananunua mazao kwa bei ya chini na kwenda kuuza kwa bei kubwa," alisema RC Malima.


Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa aliwataka wananchi wa mkoa wa Morogoro kuhakikisha wanalima mazao ya ziada ya biashara na mazao mbadala ili waondokane na dhana ya kwamba mkulima ni maskini.


Aliwataka wakulima hao kulima mazao kama parachichi, Cocoa na viazi mviringo ambavyo vinastawi katika wilaya ya Gairo kwa Wilaya hiyo imejaliwa kuwa na ardhi safi inayofaa kwa Kilimo kwa mazao mengi.


"Kwa utafiti wa kienyeji uliofanywa na wakulima wenyewe kwa wilaya hii ya Gairo zao la viazi mviringo vinastawi kwa wingi,"alisema.


Mkuu huyo wa Mkoa wa Morogoro aliwataka  wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Mazingira kuchangamkia fursa ya Maonesho hayo Makubwa ya Kilimo Biashara yatakayofanyika Wilayani Gairo kuanzia Oktoba 06, 2024 hadi Oktoba 12, 2024.

 

Aidha alisema maonyesho hayo yatawaleta pamoja wadau wote wanaohusika katika Mnyororo wa Thamani wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Mazingira wakiwemo Wakulima na Wafugaji , Wauzaji na Wazalishaji wa Pembejeo za Kilimo na Mifugo, Taasisi za Fedha, Taasisi za Utafiti katika Sekta ya Kilimo na Mifugo, Wasindikaji na Wafanyabiashara, Mashirika ya Serikali na yasiyo ya Kiserikali yanayojihusisha na Shughuli za Kilimo, Mifugo na Mazingira, Taasisi za Umma na Binafsi zinazotoa Huduma kwa wakulima na wafugaji ikiwemo Taasisi za Bima, Hifadhi ya Jamii, Nishati Safi ya Kupikia.


Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabiri Makame alisema zaidi ya asilimia 95 ya Wananchi wa Gairo wanajishughulisha katika Sekta ya Kilimo na Mifugo hivyo Sekta hizi ndiyo muhimili wa kukuza Pato la Mwananchi mmoja mmoja, kukuza uchumi wa Wilaya na Kuongeza Ukusanyaji wa Mapato ya ndani ya Halmashauri.

 

Aidha, Maonyesho  haya yatatanguliwa na Mikutano muhimu miwili ya Wakulima na Wafugaji ambayo ni 𝐒𝐀𝐌𝐈𝐀 𝐌𝐈𝐅𝐔𝐆𝐎 𝐅𝐔𝐑𝐒𝐀 𝐅𝐎𝐑𝐔𝐌 𝐮𝐭𝐚𝐤𝐚𝐨𝐟𝐚𝐧𝐲𝐢𝐤𝐚 𝐒𝐞𝐩𝐭𝐞𝐦𝐛𝐚 19, 2024 𝐧𝐚 𝐒𝐀𝐌𝐈𝐀 𝐊𝐈𝐋𝐈𝐌𝐎 𝐅𝐔𝐑𝐒𝐀 𝐅𝐎𝐑𝐔𝐌 – 𝐇𝐎𝐑𝐓𝐈𝐂𝐔𝐋𝐓𝐔𝐑𝐄 (𝐌𝐁𝐎𝐆𝐀𝐌𝐁𝐎𝐆𝐀 𝐍𝐀 𝐌𝐀𝐓𝐔𝐍𝐃𝐀).


Mikutano hii itatoa fursa kwa wakulima na wafugaji kujadiliana, kujengewa uwezo na kubadilishana uzoefu wa mbinu Bora na Teknolojia za Kisasa katika Ufugaji na Sekta ya Kilimo Cha Mbogamboga na Matunda ikiwemo zao la Parachichi na Viazi Mviringo.


Hatua hii ni utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuleta Mageuzi katika Sekta ya Kilimo na Mifugo kupitia Mkakati wa Ajenda 10/30 ambao unalenga kuongeza Kasi ya ukuaji  wa Sekta ya Kilimo kufika Asilimia 10% mwaka 2030 kutoka Asilimia 4.2 Mwaka 2023.


Maonesho ya “SAMIA KILIMO BIASHARA EXPO 2024” yamebeba ajenda Kuu 5 ambazo ni Ushiriki wa Wananchi Katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Kilimo na Ufugaji wa Kibiashara, Nishati Safi ya Kupikia na Fursa ya Biashara ya Kaboni, Afya na Lishe, Ushirika na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. 


Maonyesho haya yamebeba Kauli Mbinu isemayo 'TUNZA MAZINGIRA NA SHIRIKI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA KWA MAENDELEO YA KILIMO NA MIFUGO'


Mwisho.

No comments: