MIKUMI KUONGEZA MALANGO MATATU YA KUPOKEA WATALII LIKIWEMO LA WATAKOTUMIA RELI YA SGR - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday 1 September 2024

MIKUMI KUONGEZA MALANGO MATATU YA KUPOKEA WATALII LIKIWEMO LA WATAKOTUMIA RELI YA SGR

 

Waziri wa Maliasili na Utalii balozi Dk Pindi Chana 

Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Uhifadhi za Taifa TANAPA Musa Kuji 




Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


WIZARA ya Maliasili na Utalii imepanga kuongeza malango matatu ya kupokelea watalii watakaoingia hifadhi ya taifa ya Mikumi kwa njia ya reli ya ya kisasa ya mwendokasi (SGR) kupitia kituo cha reli hiyo ya SGR kilichopo mji wa Kilosa mkoani Morogoro.


Waziri wa Maliasili na Utalii balozi Dkt. Pindi Chana alieleza hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya toka kuanzishwa kwa Hitadhi ya Taifa ya Mikumi mwaka 1964.


Alisema ujenzi wa malango hayo utaleta chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Wilaya Kilosa hususan kwa vijiji vya Myombo, Mbamba na Kilangali na kwamba kwa sasa lipo lango moja tu ambalo limeluwa likitumika kupokea watalii.


Waziri Dk Chana alisema ujenzi huo wa Malango utaenda sambasamba na kuongeza miundombinu msingi ikiwemo upanuzi wa uwanja wa ndege uliopo hivi sasa na kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo ya Maliasili na Utaliii itaendelea kuimairisha Uhifadhi nchini kwa kuimarisha ulinzi wa maliasili ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa.


“Hifadhi hii ya Mikumi inaendelea kuimarishwa kila mara na tunaendelea kuoanua eneo la viwanja vya ndege, tunaendele kuongeza mageti ili wananchi wanaoingia katika hifadhi wasitumie lango moja tu na sasa kutakuwa na malango yasiyopungua matatu,” alisema Waziri balozi Dk Pindi Chana.


“Katika kuendeleza maboresho tutaendelea kushirikiana na wananchi waishio jirani na Hifadhi za Taifa ili kuzilinda hifadhi hizi kwa faida ya kizazi cha sasa na kile kijacho,”alisema Waziri balozi dk Pindi Chana,”alisema.


Aidha Waziri huyo alisema Hifadhi za Taifa zimeendelea kutoa mchango kwenye maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini ambapo kwa sasa Sekta ya Utalii inachangia takribani asilimia 17 ya pato la Taifa, asilimia 25 ya fedha za kigeni na ajira rasmi na zisizo rasmi zaidi ya milioni 2.


Pia alieleza kuwa mafanikio kwenye Sekta ya Utalii kwa sehemu kubwa yamechangiwa na jitihada zinazofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,kwa kutangaza utalii kupitia filamu maarufu ya ‘The Royal Tour’ pamoja na filamu ya The Amazing TANZANIA ambazo zimekuwa chachu ya kukuza utalii na kuongeza idadi ya wageni wa ndani na nje ya nchi.


Kufuatia jitihada hizo  mwaka wa fedha 2023/2024 idadi ya watalii wa kimataifa waliofika nchini imeongezeka kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 Mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,808,205 Mwaka 2023.na kwa mwaka 2023/2024 jumla ya watalii 138,844 wametembelea Hifadhi ya Taifa Mikumi sawa na ongezeko la asilimia 198.48 kutoka watalii 46,517 waliotembelea hifadhi hiyo kwa mwaka 2020/2021.


Waziri alisema mafanikio haya yameendelea kupatikana kutokana na juhudi za wadau wa Uhifadhi, Wananchi na Serikali kwa ujumla katika kulinda maliasili.


Aidha katika kuboresha miundombinu ya utalii ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi, Serikali kupitia Mradi wa REGROW inaboresha uwanja wa ndege kuwa wa kisasa katika eneo la Kikoboga, ujenzi wa malango ya watalii eneo la Doma na Kikwaraza, ujenzi wa kituo cha kutoa taarifa kwa wageni (VIC), kambi za kupumzikia wageni (Picnic Sites), maeneo ya malazi (Cottages & Campsites) na kuunganisha Hifadhi ya Taifa Mikumi kwenye umeme wa Gridi ya Taifa.


Miradi itakapokamilika itawezesha kuongeza idadi ya watalii kwa kuwa ndege kubwa zaidi zitaweza kutua ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi ambapo kwa wakati mmoja na wageni zaidi ya 140 wataweza kuhudumiwa kwa pamoja.


Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Uhifadhi za Taifa TANAPA Musa Kuji alisema wameendelea kuingiza fedha nyingi kutokana na ongezeko la watalii tangu ujio wa filamu ya Royal Tour, huku akieleza kuwa watumishi wa Tanapa wanaendele kuishi ndani ya kiapo kwa kuzilinda hifadhi zote za taifa.


Mkuu wa hifadhi wa Mikumi, kamishna msaidizi wa uhifadhi Augustine Masesa alisema changamoto mabadiliko ya tabia nchi, ujangili imekuwa changamoto lakini pamoja nachangamoto hiyo wataendelea kufanya kazi kwa uaminifu,ubunifu ikiwa ni pamoja na kulinda hifadhi na kuwanufaisha wanajamii moja kwa moja.


Wadau mbalimbali wa walioshiriki maadhimisho hayo na kudhamini walizungumzia mchango wa sekta ya utalii ambapo walisema watalii ni vyema wakatumia mawasiliano ya kidigitali wanapohitaji kufika hifadhi ya Mikumi kwa ajili ya kufanya utalii.


Mkurugenzi wa Banki ya CRDB Morogoro Joel Mageni alisema wao kwa sasa wapo digito hivyo watalii wasitembee na fedha mifukoni watumie mashine za kielektroniki kulipia kwani njia rahisi na haraka.


Naye Meneja uhusiano Banki ya Azania Arthur Nyandindi alisema wao wataendele kushirikiana na hifadhi za taifa nchini na wadau wanaohusika na sekata ya utalii katika kuhakikisha wanatangaza utalii ndani na nje ya nchini.


Hifadhi ya taifa ya Mikumi ni kongwe ambayo ni Hifadhi ya Taifa ya tano kuanzishwa baada ya Hifadhi za Taifa za Serengeti (1951), Ziwa Manyara (1960), Arusha (1960) na Ruaha (1964).


Mwisho.

No comments: