MTPC YAUNGANA NA WADAU KUADHIMISHA SIKU YA USAFI DUNIANI 2024. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 21 September 2024

MTPC YAUNGANA NA WADAU KUADHIMISHA SIKU YA USAFI DUNIANI 2024.

 





Na Mwandishi Wetu, Maipac 


maipacarusha20@gmail.com 


Waandishi wa Habari Mkoani Mtwara, wameungana na wadau wengine wa mazingira kuadhimisha siku ya usafi Duniani, kwa kushiriki kufanya usafi katika soko la Ferry Mjini Mtwara.


Zoezi hilo ambalo limeandaliwa na Chama cha waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani limelenga kuhamasisha usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali.


Wadau wengine walioshiriki kwenye zoezi hilo ni Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira-NEMC, Taasisi ya Uhifadhi wa Bahari na maeneo tengefu (Marine Park), wafanyabiashara wa soko la Ferey Mtwara na wananchi wengine. 



Akizungumzia zoezi hilo,Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Shadida Ndile, amewataka wananchi kuzingatia usafi katika maeneo yao ili kujikinga na magonjwa mbalimbali.


Kwa upande wake Maguri Wambura ambaye ni Afisa kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC Kanda ya kusini, amewakumbusha wananchi kutunza mazingira kwa kupunguza matumizi ya kuni wakati wa kupika,na badala yake watumie nishati safi.


Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Afisa Afya wa Manispaa ya Mtwara Bi. Angelina January amewasisitiza wananchi kuchukua tahadhari ya Ugonjwa wa homa ya Nyani  (Mpox) ambao umeripotiwa katika baadhi ya nchi barani Afrika.


"Pamoja na zoezi hili la usafi,lakini pia tunatumia nafasi hii kukumbushana juu ya kuchukua tahadhari ya maambukizi ya homa ya nyani, na tunawashukuru walioandaa tukio hili kwa kuweka kipengele hiki cha elimu ya Afya "


Katibu wa waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwraa Bryson Mshana, ameeleza kuwa zoezi hilo ni muendelezo wa shughuli mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na waandishi wa habari katika mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya kuwahudumia wananchi.


"Kazi ya vyombo vya habari ni pamoja na kuandaa kampeni kama hizi za usafi wa mazingira, zinazowashirikisha wananchi moja kwa moja kwa lengo la kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali yenye manufaa kwa jamii na Taifa" ameeleza Mshana




No comments: