SERIKALI Iboreshe Sheria ya Madini ili Kuondoa Migogoro Mirerani - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 27 September 2024

SERIKALI Iboreshe Sheria ya Madini ili Kuondoa Migogoro Mirerani

 







Na: Mussa Juma,Mirerani


mussasiwa@gmail.com


Eneo la Kilomita za mraba 15  lilipo Mirerani wilaya ya Simanjiro mkoa wa Manyara ni eneo pekee duniani, ambapo yanachimbwa madini  ya Tanzanite moja ya madini ghali ya vito Duniani.


Katika machimbo ya  Madini haya kumekuwepo na migogoro kila kukicha na uchunguzi wa kina wa mwandishi habari hizi umebaini miongoni mwa vyanzo vya migogoro ni sheria ya madini ambayo haiwezi kutekelezeka katika machimbo ya tanzanite Mirerani.



Madini haya yaligunduliwa  rasmi mwaka 1966 na Jumanne Ngoma mtafutaji madini kutoka eneo la Makanya wilayani Same mkoani Kilimanjaro.


Uchunguzi rasmi wa kwanza wa madini haya, ulifanyika Septemba 23 mwaka 1967 Maabara ya idara ya madini Dodoma na baadaye mwaka 1968 madini hayo yalivuka mipaka na kwenda kuchunguzwa Marekani katika kampuni ya Tiffany na ndipo yakapewa jina la Tanzanite.


Baada ya ugunduzi huo kuthibitishwa, kati ya mwaka 1968 na 1971 serikali ilianza kuwamilikisha watu binafsi maeneo ya kuchimba madini haya.


Hata hivyo, mwaka 1971 April Mosi, serikali ilitaifisha migodi yote ya Tanzanite Mirerani na ilikabidhiwa kwa shirika la maendeleo la taifa (NDC) ambayo ilianzisha kampuni tanzu ya Tanzania Gemstone Industries Ltd(TGI).


Serikali mwaka 1972 iliunda shirika la madini ya Taifa (STAMICO) na TGI ikawekwa chini ya usimamizi wake lakini, walishindwa kulilinda eneo hilo na ndipo lilivamiwa na wachimbaji wadogo.


Katika hali ya kulidhibiti upya eneo hili julai 21mwaka 1987 serikali ililigawa eneo hili katika  vitalu vinne kwa njia ya zabuni ambapo Kitalu A chenye ukubwa wa kilomita za mraba 0.8 ilipewa kampuni ya Kilimanjaro  Mines Ltd.


Kitalu B, chenye ukubwa wa takriban kilomita za mraba 1.31 kilitolewa kwa kampuni ya Building Utilities na  baadaye kutokana na vurugu, wakaja kupewa wachimbaji wadogo.


 Eneo la Kitalu C lenye  ukubwa wa kilomita za mraba  7.6 walipewa kampuni ya Graphtan Ltd  iliyokuwa na ubia na TGI na Samax 


Mwaka 1999  Kampuni ya Graphtan  Ltd iliyokuwa inachimba kitalu C chenye eneo kubwa  nusu ya eneo lote la Mirerani, iliwekwa chini ya mufilisi kutokana na kushidwa kulipa mkopo wa PTA Bank na ndipo mwaka 2005  kampuni ya Afrika Gem (AFGEM) ya Afrika Kusini ilinunua eneo hilo na baadaye kuliuza kwa kampuni ya Tanzanite One ya nchini Uingereza kwenye soko la hisa.


Migogoro iliendelea katika kitalu hiki   Tanzanite One nao walikwama kuchimba kwa "raha" baada ya migogoro kuwa mingi na wachimbaji wadogo walijiondoa kuchimba na wakakodishiwa na serikali kitalu hiki Kampuni ya wazawa ya Sky associate wakishishiriana na STAMICO.


Licha ya Sky Associate na STAMICO kufanya kazi kubwa kurejesha mahusiano na wachimbaji wadogo migogoro iliendelea nao wakajiweka kando na serikali sasa imekitoa Kitalu hiki kwa kampuni ya Franoni ambayo inamilikiwa na wazawa.


Katika machimbo haya kuna eneo la kitalu D  lenye migodi 368 ya wachimbaji wadogo awali walipewa chama cha wachimbaji wadogo Arusha (AREMA) na baadaye kutokana na migogoro mwaka 1992 kiligawaywa kwa  wachimbaji wadogo.


Kuna eneo jingine la  kitalu D la ukubwa la kilomita za mraba 0.043  lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya  Osoit pusu Ltd, eneo la kilomita za mraba 0.003 linamilikiwa na  kampuni ya Gem& rock Venture, eneo la 0.59 kilomita za mraba linamilikiwa na J.S Magezi& Sons.


Wamiliki wengine ni kampuni ya Tanzanite Afrika Ltd, ina eneo la kilomita za mraba 0.19, Gem &Rock Venture 0.28 na Paradiso Minerals Ltd wana eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 0.41.


Chanzo cha kuibuka migogoro Mirerani 


Mwaka 1995 kutokana na hali ya kisiasa, serikali iliifutia umiliki wa kitalu B kampuni ya Building Utilities na kuwapatia eneo hilo wachimbaji wadogo ambao kila mmoja alipewa eneo la kuchimba mita 50 kwa 50 .


Uamuzi huu ambao ulikuwa wa kisiasa hadi sasa unaigharimu Mererani na ndio unaisukuma serikali kufanya maboresho ya sheria ya madini kwa kuja na sheria maalum kwa madini ya vito pekee.


Mwenyekiti mstaafu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (MAREMA) Sadiki Mnenei anasema tanzanite haichimbwi kama dhahabu ama choo kwa kwenda chini mita 50 pekee.



"Hapa ndipo kwenye kiini cha mgogoro haiwezekani sheria hii ya madini iseme mchimbaji achimbe mita 50 kwa 50 "anasema


Mnenei ambaye ni mchimbaji mdogo anashauri serikali kuona umuhimu wa maboresho ya sheria ili kuondoa migogoro mirerani na pia kupoteza mitaji ya wachimbaji wadogo.


Mwenyekiti mstaafu na chama cha wachimbaji wadogo migodi ya tanzanite Mirerani Wariamangi Sumari anasema kama serikali inataka Mirerani itulie lazima ibadili sheria ya madini.


"Hii sheria yao haitekelezeki na kama ikifuatwa wachimbaji wote Mirerani migodi yao itafungwa kwani wapo nje ya lesseni zao"anasema


Anasema kila kukicha migodi ya wachimbaji wadogo inafungwa ama kulazimishwa ubia kwa madai ya kuingia eneo la kitalu C.


Anasema wamepeleka maelezo yao serikali na kutoa maoni katika tume mbalimbali ambazo zilitumwa Mirerani na kubwa ni maboresho ya sheria lakini serikali haijachukuwa hatua.


Akizungumzia athari za migogoro Mererani mfanyabiashara wa madini  Herieth Evarist Mushi, amesema kuwa wameshindwa kuwapeleka watoto shule baada ya mji wa Mirerani kufa kwani watu hawana ajira na wamekosa madini kutokana na mgogoro wa mipaka.

Anasema  anasema kama Serikali ikiboresha Sheria na kuruhusu uchimbaji kwa kuzingatia Sheria za usuluhishi kama ilivyo kitalu B na D migodi mingi itaendelea na kazi na hivyo kutoa Madini ambayo yatawanufaisha wanawake pia.





Kanaeli Minja alisema mji wa Mirerani unategemea  wachimbaji wadogo lakini tangu baadhi ya  migodi yao kufungwa kwa tuhuma za kuchimba eneo la kitalu C, maisha yamekuwa magumu sana Mererani.


“Tunalia na Rais Samia kwani tunajua kuna watu wapo nyuma ya migogoro hii, tumeomba sheria ya madini kuboreshwa lakini maombi yanapuuzwa.


Alisema wanawake wa Mererani ndio waathirika wakubwa wa migogoro kwani hali ya maisha inakuwa ngumu,wanaume wengi wametelekeza familia kutokana na haki ngumu ya maisha.


Kupotea umaarufu wa Mirerani


Machimbo ya Tanzanite Mirerani, yalikuwa ni kimbilio kubwa kwa vijana, kutokana maeneo mbali mbali nchini miaka ya 1990 hadi 2010 na zaidi ya watu 30,000 walikuwa katika eneo hilo.


Mamia ya vijana hawa  walikuwa wakifika Mirerani kuchimba madini ya Tanzanite, wengine wakinunua na kuna maelfu ambao walikuwa wakifanyakazi ya kuchekesha michanga (wanaapolo)  kutafuta madini.


Hakika wote waliweza kupata riziki zao na ndio sababu hata serikali ilipotangaza mara kadhaa kuwataka vijana wasio na kazi katika migodi kuondoka Mirerani, jambo hili lilikuwa gumu.


Hata hivyo, mambo yalianza kubadilika kuanzia mwaka 2010 baada ya uchimbaji kuimarika na kuanza kutoa faida kubwa kwa wachimbaji wadogo na wawekezaji.


Upanuzi wa migodi mingi ulifanyika lakini hapo hapo, kutokana na kushamili uchimbaji, migogoro ilianza baina ya wachimbaji wadogo na wawekezaji.


Wakati huo, wengi watakumbuka kuundwa kwa kamati mbali mbali za usuluhishi hasa kutokana na mwekezaji kuonekana ni tishio Mirerani kutokana na kuwa na ulinzi wa hatari wa mbwa kila kona na nyaya za umeme ikiwa ni kinyume cha taratibu.


Katika kipindi hiki, ndipo wizara ya Nishati na madini, ikaja na mapitio ya sheria na uchimbaji madini ya mwaka 1998, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004 na baadaye   mwaka 2010 kifungu cha 55(3) ambacho kinalazimisha kuchimba madini haya kwenda chini kulingana na leseni.


Katika sheria hii mchimbaji anatakiwa kuchimba madini katika eneo lake la leseni tu, hivyo kwa mamia wenye leseni za kuchimba eneo lao la  mita 50x50 ina maana ni wazi uchimbaji wao utakoma kwani wakivuka nje ya eneo lao wanakabiliwa na tishio la kufungiwa.


Licha ya sheria hii kupingwa na wachimbaji wadogo, kupitia vyama vyao vya wachimbaji, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) lakini serikali imesimamia ni lazima itekelezwe.


Katika uchunguzi maalum, mwandishi habari hii  Mirerani kwa kuwashirikisha wachimbaji wadogo, viongozi wa serikali ngazi mbali mbali, vyama vya wachimbaji na wauzaji wa madini, NG0s zinazohusika na madini, imebainika kuwa sheria ndio chanzo cha migogoro  Mirerani.


Jonas Laizer ni mchimbaji mdogo Mirerani, anasema miaka ya nyuma kabla ya kuanza kutumika sheria mpya, wachimbaji walikuwa wakipata madini, kutokana na kuchimba kwa kufuata miamba lakini sasa sheria inazuia.



Anasema anayenufaika na sheria hii ni mwekezaji kitalu C kwani ndiye anamiliki karibu nusu ya eneo zima la madini Merelani ambalo ndipo kitovu cha madini.


Laizer anasema wachimbaji wadogo, maeneo yao mengi ni madogo kwa mfano eneo la kitalu B  waligaiwa kila mmoja mita 50 kwa 50 hivyo, kwa sheria ilivyo huwezi kuchimba madini.


 

Anasema miamba ya Mirerani, mseleleko wake ni eneo la kitalu C ambalo ndipo kunachimbwa na mwekezaji na ambaye analeseni kuchimba peke yake.


Anasema asilimia zaidi ya 50 ya migodi ya kitalu B na D tayari imeingia  chini kwa chini zaidi ya mita 500 eneo la kitalu C hivyo Sasa kutaka warudi nyuma ama kuchimba kwa ubia ni tatizo.


"Ndiyo sababu tunasema hapa sheria inawabeba wawekezaji, kwani wanaeneo kubwa ambalo ndipo miamba ya midini inaelekea na kuzuia kuchimba kwa kufuata miamba na kutuondoa sisi katika uchimbaji"anasema 


Aliyekuwa Katibu wa chama cha wachimbaji wadogo mkoa wa Arusha (AREMA) kwa muda mrefu Isaya Letema  anasema walipeleka malalamiko yao, serikali hadi kamati ya bunge inayohusika na madini lakini walikwama.


Anasema mara ya mwisho wamefikisha malalamiko rasmi kwenye kamati ya bunge hasa baada ya tishio la kufungwa migodi 19 inayopakana na kitalu C .


Letema alisema kimsingi wanachotaka wachimbaji wadogo ni kuwa zifuatwe sheria za usuluhishi migodini ambazo zimedumu kwa zaidi ya miaka 20 katika maeneo ya kitalu B na D.


Mchimbaji Lenganasa Soipei anasema, sheria ya madini ya mwaka 2010 kifungu cha 55(3) inapaswa kufanyiwa marekebisho kwani kwanza wachimbaji wadogo hawakushirikishwa ili watowe uzoefu wao.


“Sheria hii inatumika kwenye machimbo ya dhahabu na almasi sio Tanzanite ambayo inachimbwa kwa kufuatwa miamba”anasema 


Mchimbaji huyo ambaye anamiliki mgodi ya unaopakana na kitalu C anasema ndio sababu sasa serikali inalazimisha ubia kwani kimsingi sheria yake haitekelezeki.

Anasema kwa kutaka kusimamia sheria hiyo ni kutaka kuwaondoa wachimbaji wadogo, Mererani kwani kwa jinsi walivyopewa maeneo yao hakuna hata mmoja ambaye anachimba ndani ya leseni.


“kuwaondoa wachimbaji hapa ni kusababisha maafa kwa familia zao na taifa zima kwani watu zaidi ya 10,000 wakikosa kazi sijuwi wao na familia zao watategemea nini”anasema 




Mchimbaji Seniniu Laizer maarufu kama Bilionea Laizer, mmoja wa wachimbaji wadogo, maarufu  nchini anasema sheria hiyo ya madini inatumika vibaya na hadi sasa imemsababishia hasara ya zaidi ya millioni 500.

"Bado tunaiomba serikali kufanya maboresho ya sheria ya uchimbaji madini ya vito ili kumaliza migogoro Mererani"anasema


“Hata mgodi wangu ambao ulikuwa katika uzalishaji umesimama muda mrefu kutokana na migogoro ya mipaka na kitalu C ”anasema


Mchimbaji Ismail  Kaaya anasema pia kupewa mwekezaji mmoja kumiliki eneo la kilomita za mraba 7.6  ni makosa kwa mujibu wa kanuni za uchimbaji madini ya vito aya ya 5(1)(f) ambayo inasema ukubwa wa mwisho wa eneo utakuwa kilomita moja ya mraba.


“Pia hata hii sheria ambayo imesababisha migodi kufungwa ilikuwa haituhusu sisi kwani imetungwa wakati tayari tumekuwa tumeingia chini eneo hilo la kitalu C kwa kuwa hakukuwa na sheria za kuzuia kutoingiliana chini ya migodi”anasema.


Hali ya uchimbaji Mirerani.      

 Kati ya migodi 551 inayochimbwa katika maeneo ya kitalu B na D ni migodi isiyozidi 120 ambayo ndio inachimbwa kikamilifu kwa sasa.


Waziri wa Madini, Anthony Mavunde


Maelezo ya wizara ya Nishati na madini.


Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akizungumza mara kadhaa kuhusiana na migogoro Mererani amekuwa akisisitiza uchimbaji kufuata sheria.


Hata hivyo Mavunde anakiri kama sheria ikifuatwa kama ilivyo migodi mingi inafungwa Mererani.


"Ili kutatua migogoro lazima tutangulize pia busara zetu ili kuhakikisha uchimbaji unafanyika kwa usalama Mirerani na taratibu za kisheria zinafuatwa"alisema.


Alisema kimsingi  haiwezekani mtu mwenye leseni ya madini kuchimba madini nje ya leseni kwani jambo hilo halipo duniani na hakuna ukiukwaji wa sheria kutokana na msimamo wa wizara.




Nini  ushauri wa Tume za Mirerani kutatua migogoro.


Tume ya Jaji Mark Bomani na  aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Generali  Robert Mboma ya mei 2002  ziliwahi kupendekeza  kuwa madini ya Tanzanite yachimbwe na wachimbaji wadogo pekee kwa kuwa hayana ushindani katika soko la kimataifa.


Tume hiyo ya Mboma pia  ilipendekeza ili litatuliwe tatizo la mipaka baina ya kitalu B na C na kurejesha mipaka ya mwanzo wa mwaka 1987 na pia serikali isitishe  leseni katika eneo la kitalu C kwa mwekezaji mkubwa  na iwawezeshe wachimbaji wadogo kuchimba madini katika eneo hilo kwa utaratibu maalum ambao utawekwa.


Mussa juma ni mwandishi mwandamizi wa habari   mkoa wa Arusha anapatikana Email: mussasiwa@gmail.com 

0687001700 /0754296503


Mwisho

No comments: