WATU WANNE WASHIKILIWA KWA MAUAJI YA DEREVA BODABODA KILOMBERO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 10 October 2024

WATU WANNE WASHIKILIWA KWA MAUAJI YA DEREVA BODABODA KILOMBERO

 



Na: Lilian Kasenene,Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


WATU wanne wanashikiliwa na Polisi mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za mauaji ya Shaban Mwawile(18)bodaboda mkazi wa Lipangalala Wilaya ya Kilombero na kisha kumpora pikipiki yake.


Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Alex Mkama alisema hayo Leo ofisini kwake wakati akizungumza na waandishi wa habari.


Mkama alisema tukio hilo lilitokea Septemba 8,2024 mwaka huu Kilombero ambapo awali zilitolewa taarifa na ndugu kuwa kijana huyo amepotea na ndipo jeshi la Polisi lilipoanza ufuatiliaji na ilipofika Septemba 29,2024 watuhuma wote wanne walikamatwa kuhusiana na mauaji hayo.


Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni 

Athuman Mpango(38) fundi ujenzi mkazi wa Ifakara, Denis Swai(34)mkulima mkazi wa Mofu, Mussa Bushiri(28) mkulima mkazi wa Upogoroni na Alhaji Likwaya (32)mkulima mkazi wa Michenga.


Alisema watuhumiwa hao baada ya kufanyiwa mahojiano ya kina walikiri kuhusika na tukio la mauaji la kijana huyo na kisha kuwaongoza askari mpaka kwenye kambi ya Senga iliyopo katika pori la akiba la Kilombero kata ya Minepa Wilaya ya Ulanga walipoutelekeza mwili wa  bodaboda huyo ambapo ulikutwa umeharibika.


Kamanda Mkama alisema upelelezi wa tukio hilo unaendelea na watafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika.


Katika tukio lingine, Polisi Morogoro wamemkamata Said Mada(28) mkazi wa kijiji cha Malui kata ya Tindiga Wilaya ya Kilosa na wenzake watatu kwa tuhuma za kuhusika na tukio la unyang'anyi wa kutumia silaha.


Tukio hilo lilitokea Agosti 7,2024 usiku katika kitongoji cha Makale Magole tarafa ya Turiani Wilaya ya Mvomero ambapo walimvamia Kulwa Magale(49)mfanyabiashara wa Kokoa akiwa nyumbani kwake.


Alisema watuhumiwa hao walitumia silaha inayosadikika kuwa ni Gobole pamoja na panga na kumnyang'anya kiasi cha sh 20 milioni.


Watuhumiwa hao pia walikamatwa wakiwa na silaha aina ya shortgun na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.


Aidha kamanda Mkama amesema watuhumiwa 35 wanaohusika na wizi wa mitandaoni wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa wakiwa na posi sita, simu Moja ya kusajilia na laini 1979 zikiwa tayari zimesajiliwa kwa majina tofauti na kuziuza laini hizo za makampuni mbalimbali ya mitandao ya simu kwa matapeli wengine.


Kamanda Mkama alisema Jeshi hilo katika mkakati wake wa kuzuaia utapeli unaohusisha mitandao ya simu lilifanya msako maalumu dhidi ya watu wanaopita kwenye mitaa mbalimbali katika wilaya za Kilombero, Malinyi, , Morogoro na Mvomero.


Alisema watuhumiwa walikuwa walitumia namba za NIDA za watu mbalimbali na kuzalisha usajili wa laini zaidi ya Moja bila ridhaa au utambuzi wa wamilikinwa vitambilisho vya NIDA.


Alieleza kuwa katika Wilaya ya Kilombero walikamatwa watuhumiwa 18, Manispaa ya Morogoro watuhumiwa 8, ambapo watuhumiwa watatu kati ya hao ni vinara wa utapeli ambao walikamatwa eneo la Ifakara wakiwa tayari wametumia laini hizo na kujipatia zaidi ya Sh. 9 milioni kutoka kwa watu mbalimbali kote nchini.


Kamanda Mkama alitoa ushauri kwa wananchi kuacha kufanya usajili kwa watu wasiowafahami na kutokuwa na vitambulisho vya NIDA ambapo aliwataka wananchi kutafuta riziki kwa njia ya halali kwa sababu uhalifu haulipi na mwisho wake ni kukamatwa na kuishia jela.


Mwisho.

No comments: