SAT YAWAJENGEA UWEZO WAKULIMA NA WAFUGAJI SIMANJIRO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 26 November 2024

SAT YAWAJENGEA UWEZO WAKULIMA NA WAFUGAJI SIMANJIRO

 


Na Mwandishi wetu, Simanjiro


maipacarusha20@gmail.com 


SHIRIKA la kilimo endelevu Tanzania (SAT) limewajemgea uwezo wafugaji na wakulima zaidi ya 10,000 wa vijiji 10 vya wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wa kutokomeza udumavu, matumizi ya mbinu za kilimo ikolojia, usimamizi bora wa malisho kwa mifugo na lishe ya mama na mtoto.


Wafugaji na wakulima wa vijiji vya Kandasikira, Nadonjukini, Kiruani, Ruvu Remiti, Kambi ya Chokaa, Naberera, Lemkuna, Narakauwo, Orkirung’rung’ na Ngage, wamepata mafunzo hayo kupitia shirika la kilimo endelevu Tanzania (SAT), kwa ufadhili wa shirika la mpango wa chakula duniani (WFP).


Mwezeshaji kutoka SAT, Yohana Malecela, akizungumza kwenye kijiji cha Kandasikira kata ya Shambarai, amesema zaidi ya watu 10,000 wa vijiji 10 wamejengewa uwezo huo.


Malecela amesema wakulima na wafugaji hao wamenufaika na elimu hiyo kupitia mradi wa urejeshaji wa kilimo ikolojia (Muki), kutokomeza udumavu, matumizi ya mbinu za kilimo ikolojia, usimamizi bora wa malisho kwa mifugo na lishe ya mama na mtoto.


Amesema wamefanikiwa kuwajengea uwezo wananchi hao wa vijiji 10 wakiwemo wanaume 4,965, na wanawake 5,035 na watanufaika kupitia mradi huo, utakaotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja 2024/2025.


“Lengo la mradi ni kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji juu ya mbinu endelevu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, mbinu za kilimo ikolojia, matumizi ya teknolojia za uhifadhi wa maji  na udongo na kufanya urejesho wa rasilimali zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi,” amesema.


Amesema wamefikia hatua ya kutekeleza mradi huo, kutokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa la athari za mabadiliko ya tabianchi katika jamii ikiwamo mvua kutokunyesha kwa utaratibu uliozoeleza, kupungua kwa mavuno ya chakula na uhaba wa malisho ya mifugo.


“Baada ya kutekezwa kwa mradi kumekuwapo na mabadiliko chanya kwa sehemu inapotekelezwa kwani wakulima na wafugaji wameanza kutumia elimu ya kilimo ikolojia kwa manufaa zaidi,” amesema Malecela.


Hata hivyo amsema wakulima na wafugaji wamefanikiwa kuunda vikundi 221 ambavyo kupitia shughuli hizo, wameanza kuweka akiba ya fedha na kukupeshana na kutumia vikundi hivyo kupeana elimu.


“Kupitia mradi wa Muki ili kuweza kuwafikia wakulima na wafugaji 10,000 tulitoa mafunzo kwa wakulima wawezeshaji (wakulima viongozi) ambao tunawatumia kama wawezeshaji jamii 300 katika vijiji vya mradi na kila kijiji tulichagua wakulima na wafugaji 30 waliojifunza na kwenda kutoa elimu kwa wenzao,” amesema.


Mwezeshaji mwingine wa SAT, Lucy Shija, amesema kilimo ikolojia kina manufaa kwa wakulima kwani wanatumia mbolea na dawa za asili ikiwemo mboji, pilipili na alovera.


“Wakulima wanapaswa kuepuka matumizi ya  kemikali kwa uzalishaji wa mazao na endapo shughuli za kilimo zisipofanyika vyema kuna uwezekano wa walaji wa chakula kupata madhara,” amesema Shija.


Amesema kilimo ikolojia ambacho ni cha asili kikitumika kitasaidia kuboresha suala la lishe kwani itasaidia kuepusha watu kutumia vyakula vilivyotumia kemikali nyingi.


Ameeleza kuwa kilimo hicho kitawasaidia watu kuboresha namna ya upatikanaji wa chakula kwani kitapatikana kwa wingi na kitakuwa salama kwa matumizi ya bianadamu.


“Kupitia kilimo hiki watu watapata vyakula mchanganyiko, kuboresha afya ya mama na mtoto na itasaidia kupunguza udumavu kwa watoto kwa kutopatiwa chakula cha aina moja kila mara,” amesema.


Afisa lishe wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Eshimuni Swai, amewataka wanawake wa eneo hilo kuwanyonyesha watoto wao kwa muda wa miezi sita bila kuwapa chakula kingine kwani maziwa ya mama ni lishe tosha.


“Maziwa ya mama yana maji na maziwa hivyo nyonyesheni bila kuwapa chochote hata maji au uji, kwani ziwa la mama ni mlo kamili wa mtoto, mradi mzazi ale vizuri ili maziwa yatoke,” amesema Swai.


Mkazi wa kijiji cha Kandasikira Filbert Mianga, amesema kupitia elimu hiyo watakuwa wanatumia mbolea za asili ikiwemo samadi na mboji na kuepuka kutumia viuatilifu vyenye kemikali.


Mianga amesema elimu iliyotolewa imeleta matokeo chanya kijijini hapo, kwani wafugaji na wakulima wameanza kutumia mbinu za kilimo ikolojia na lishe bora kwa mama na mtoto.


Mwisho wa mafunzo hayo wakazi wa kijiji hicho walioshiriki mafunzo hayo walipatiwa uji wenye lishe na ndizi kwa lengo la kupata elimu ya vitendo kuhusu suala la lishe bora.


MWISHO

No comments: