Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase |
Na: Julieth Mkireri , Maipac Kibaha
maipacarusha20@gmail.com
SIKU tisa baada ya tukio la utekeji mtoto wa miezi saba huko Galagaza kata ya Msangani Wilaya ya Kibaha hatimaye amepatikana akiwa hai na watekaji watatu kati ya wanne wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase amesema mtoto huyo amepatikana katika msitu wa Kimaramisale na Serengeti B kata ya Dutumi Wilaya ya Kipolisi Mlandizi watuhumiwa hao wakiwa wamejificha na mtoto kukwepa msako.
Kamanda Morcase amesema watuhumiwa hao walikamatwa usiku wa saa tisa Januari 24 wakiwa na mtoto huyo wa kike waliyemchukua katika tukio la uvamizi lililotokea Januari 15 huko Galagaza kata ya Msangani Wilaya ya Kibaha.
Katika eneo hilo pia polisi walifanikiwa kukamata gari lenye usajili wa namba T 331 DLZ Toyota ist iliyoibiwa katika tukio hilo.
Watuhumiwa hao walikutwa na Pete ya ndoa ya mke wa Melkisedeck Mrema, simu moja, kompyuta mpakato moja kati ya tatu zinazodaiwa kuibiwa.
Kamanda Morcase amesema taratibu za upelelezi wa tukio hilo zinaendelea kwa mahojiano ya kina ikiwa ni pamoja na kumsaka mtuhumiwa mmoja ambaye hajapatikana hadi sasa.
Watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria .
Katika tukio hilo la uvamizi lililotokea Januari 15 mwaka huu watu wanne wasiofahamika walivamia nyumbani kwa Melkzedeck Sostenence Mrema mkazi wa Galagaza wakiwa na mapanga na nondo.
Katika tukio hilo watuhumiwa walimteka mtoto wa miezi saba na kuondoka nae pamoja na gari na vitu mbalimbali ikiwemo televisheni, simu na kompyuta mpakato tatu.
Kabla ya kuondoka walimtumbukiza kwenye shimo la maji taka Melkzedeck na mke wake katika mashimo mawili tofauti.
Mwisho
No comments:
Post a Comment