TUME YA RAIS YA MABORESHO YA KODI YAKUTANA NA WADAU WA BIASHARA MTWARA. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 31 January 2025

TUME YA RAIS YA MABORESHO YA KODI YAKUTANA NA WADAU WA BIASHARA MTWARA.

 





Na Mwandishi Wetu, Mtwara


maipacarusha20@gmail.com 


Wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa Biashara Mkoa wa Mtwara, wameshiriki katika kikao cha kupokea Maoni, Kero,  Changamoto na Mapendekezo kwa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi.


Mwanaidi Sinare Majaar ambaye ni Kaimu Mwenyekiti wa Tume hiyo, ameeleza kuwa Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aliunda Tume hiyo ambayo inazunguka nchi nzima ili kupata maoni ya wafanyabiashara katika kero zinazowakabili ikiwepo utitiri wa Kodi.


"Utitiri wa Kodi katika biashara ndio ulimfanya Mhe.Rais Dkt.Samia kuunda Tume ya kutazama mifumo mbalimbali ya Kodi na kuweza kutoa mapendekezo ya kufanya maboresho ya kuhakikisha kuwa kodi inakusanywa lakini pia kuondoa mzigo kwa walipakodi" ameeleza Kaimu Mwenyekiti 


Akitoa maoni katika kikao hicho,  Mwenyekiti Chemba ya wafanyabiashara wanawake Tanzania Mkoa wa Mtwara Bi.Mwajuma Ankoni ameipongeza Tume hiyo ambayo amesema itasaidi kusikiliza kero za wafanyabiashara na kuzipeleka kwa Mhe.Rais kwa ajili ya utatuzi.


Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Soko Kuu la Mtwara Mshamu Said Kaisi, ameshauri juu ya kushusha viwango vya kodi kwa bidhaa zinazotoka nchi jirani ya Msumbiji ili kuvutia wafanyabishara wengi zaidi na kuchangamsha uchumi wa Mkoa.


Aidha, kwa upande wake Mtumba said Hashimu, katibu Soko Kuu Mtwara ameshauri juu ya uanzishwaji wa mitaala ya kufundishia shuleni itakayokuwa inahusu masuala ya Kodi, ili kutengeneza kizazi kitakachokuwa na uelewa wa mambo ya Kodi ambayo hivi sasa kuna baadhi ya watu wanaona kuwa ni kero kwao.


Awali akifungua Kikao hicho Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Abdillahi Mfinanga, alisema kuwa ujio wa Tume hiyo ni fursa kwa wafanyabiashara katika mkoa huo kutoa maoni, kero,changamo na mapendekezo ya maboresho ya Kodi.




No comments: