NA: Burhani Yakub, Tanga.
maipacarusha20@gmail.com
Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Tanga ( Bombo) imeondokana na changamoto mbili za uhaba wa maji zilizokuwa zikiikabili baada ya kuchimbiwa visima vya maji safi na salama.
Changamoto hizo ni kukosekana kwa maji yanapokuwa yamekatika ambayo hutolewa huduma na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (Tanga Uwasa) na kumudu Kwa shida gharama ya sh 20.milioni za bili ya kila mwezi ya matumizi ya maji hayo.
Hayo yamebainika leo wakati asasi ya Master One Family ilipokuwa ikikabidhi kisima cha pili cha maji safi na salama kwa uongozi wa Hospitali ya Bombo kilichochimbwa nje ya jengo la wodi ya Galanos.
Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Bombo,Dr Athumani Kihara ni kuwa baada kukabidhiwa kisima hicho,Hospitali hiyo imeagiza vifaa vitakavyotumika kuunganisha miundombinu ya kutoa maji kwenye visima hivyo na kupeleka kwenye majengo mbalimbali.
"Miundombinu iliyopo ni ile ya kutoa maji ya mabomba ya Tanga Uwasa na siyo haya ya visima kwa hivyo tumeagiza vifaa vitakavyowezesha kusambaza maeneo mbalimbali maji haya yatokayo kisimani"amesema Dr Kihara.
Mratibu wa mradi wa kuchimba visima hivyo, Rahim Iliasi amesema hicho ni kisima cha pili ambapo cha kwanza kilikabidhiwa hospitalini hapo mwishoni mwa mwezi iliyopita.
"Kwa hivi visima viwili ambavyo tumevikabidhi maji yake ni mengi yenye kutosheleza matumizi ya hospitali yote kwa muda wote...tutachimba kingine cha tatu hicho kitahifadhi maji ya ziada ili kuhakikisha hayakosekani tena"amesema Iliasi.
Mratibu huyo amesema wazo la kuchimba visima hivyo lilitolewa na Mkurugenzi wa Master One Family, Asma Seif Sharji kama sadaka kwa mwanzikishi wa asasi hiyo,marehemu Suleyman.
Mkazi wa Mombo Wilayani Korogwe,Raisha Hussein amesema visima hivyo ni mkombozi kwani awali yanapokatika wauguzi na wagonjwa walikuwa wakipata shida.
"Nimeshawahi kulazwa hapa Bombo na nimeshauguza wagonjwa wodini yakikatika maji huwa inakuwa kizaa zaa lakini kwa visima hivi itakuwa ni ukombozi mkubwa"amesema Raisha.
MWISHO
No comments:
Post a Comment