Na Julieth Mkireri, MAIPAC RUFIJI
maipacarusha20@gmail.com
Madiwani Wilayani Rufiji Mkoani Pwani wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mohamed Mchengerwa kwa kutoa fedha kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 150 za ujenzi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo katika kipindi Cha miaka mitano hali iliyopelekea kutatua changamoto nyingi za Wananchi na kuifanya Rufiji kuwa miongoni mwa Wilaya zinazotambulika kimaendeleo kulinganisha na miaka ya nyuma.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Rufiji Abdul Chobo Katika kikao maalumu Cha baraza la kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kilichofanyika leo Katika ukumbi wa Halmashauri Utete.
"Sisi Madiwani wa Rufiji tunapenda kutoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo tumefanya nae kazi kwa miaka hii mitano, katuletea fedha nyingi za miradi zaidi ya bilioni 150 ambazo zimeingia Rufiji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo" amesema Chobo.
Akiwasilisha taarifa ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) ya Mwaka wa fedha 2023/2024 mbele ya Baraza la Madiwani Chobo amesema Halmashauri ya Mji Rufiji imepata hati safi huku ikifanikiwa kufuta hoja 40 kati ya hoja 49 na kuongeza kuwa hoja 9 zilizobaki zinaendelea kupatiwa majibu na kuingia katika mchakato wa kufutwa.
"Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali amejiridhisha kuwa kutokana na ushahidi wa vielelezo alivyovipitia, Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji imepata hati safi".
Aidha Chobo alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Rufiji Mhe Mohamed Mchengerwa kwa namna ambavyo anaipigania Rufiji Katika ujenzi wa miradi Katika Sekta mbalimbali ikiwemo, Barabara, umeme Vijijini, ujenzi wa vituo vya Afya na Zahanati, ukarabati wa hospitali ya Wilaya, kuvutia wawekezaji kuwekeza Rufiji pamoja na ujenzi wa Barabara ya Utete-Nyamwage kwa kiwango cha lami.
"Lakini pili tunamshukuru Mbunge wetu Mohamed Mchengerwa tumefanya nae kazi kubwa sana ya kuijenga na kuipigania Rufiji" amepongeza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Luteni Kanali Fredrick Komba, alitoa pongezi kwa Halmashauri ya Mji Rufiji kwa kupata hati safi kwa kipindi Cha miaka mitano mfululizo, huku akiwahikikishia Madiwani na Wananchi wa Rufiji kuwa Rufiji ipo salama na kuwataka kuendelea kulinda amani na utulivu ndani ya Wilaya hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashidi Mchata alitoa pongezi kwa Halmashauri ya Mji Rufiji kwa kupata hati safi huku akiwataka kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza uchumi wa Halmashauri.
Mwisho



No comments:
Post a Comment