![]() |
| WAZIRI Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa |
![]() |
| Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akizungumza na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Mussa Assad |
Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
WAZIRI Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka maafisa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini kuhakikisha ndani ya siku saba wanatoa elimu ya pamoja kwa wanafunzi kuhusu ujazaji wa fomu za mikopo kupitia mfumo wa kidigitali.
Majaliwa, ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Waislam cha Morogoro (MUM), alipomwakilisha Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Waziri mkuu Majaliwa alisema ni vyema Elimu hiyo ikatolewa kwa pamoja badala ya kusubiri malalamiko ya mwanafunzi mmoja mmoja, alisisitiza kuwa wanafunzi wengi hukosa mikopo licha ya kuwa na sifa, kutokana na makosa ya ujazaji wa fomu.
“Maafisa wa mikopo naelekeza fanyeni kazi hiyo na wala siyo zaidi ya wiki muwe mmeifanya kazi hii,"alisema.
Alielekeza wawaambie wanafunzi wakati sahihi wa kuomba mkopo ni upi ili waweze kupata mikopo hiyo na kwamba taratibu zote Serikali imeziweka wazi hakuna sababu ya mtoto wa kitanzania kushindwa kupata mkopo huo kama mwanafunzi anasifa zinazo hitajika.
Majaliwa pia aliendelea kusisitiza kuwa malengo ya mikopo ni kutaka watoto wa kitanzania wanaotoka kwenye familia mabazo zinauhitaji waende vyuoni wakasome apate elimu bila kikwazo cha ukosefu wa fedha.
Katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu alizindua rasmi Mfuko wa Jamii wa Chuo cha MUM (MUM Community Fund) kwa lengo la kusaidia wanafunzi na maendeleo ya chuo,
Katika mfuko huo alichangia Sh milioni 10 kwa niaba yake na kusoma salamu za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alichangia Sh milioni 100.
Waziri Mkuu Majaliwa akiziagiza taasisi za elimu ya juu nchini kuwekeza zaidi katika tafiti zitakazo kuja na majawabu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili watanzania ili serikali iweze kuzitafutia ufumbuzi.
Aliagiza Wizara ya elimu kuimarisha mahusiano na vyuo vyote vya elimu ya juu nchini ili viweze kutoa elimu bora kwa watanzania na kuvitaka vyuo vikuu nchini kuiga mfano wa chuo hicho katika kuwaandaa vijana kuwa na maadili na uwajibikaji
Mwaka 2005 aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamini Mkapa aliweka historia nchini kwa kutoa majengo yaliyokuwa ya chuo cha shirika la umeme Tanesco na kuyakabidhi kwa waislamu kwa lengo la kuanzisha chuo kikuu.
Miaka ishirini ya maamuzi ya kiongozi huyo yalileta mageuzi katika sekta ya elimu ya juu nchini kutoka wanafunzi 160 wakati kinaanza hadi kufikia wanafunzi 5,000kwa Sasa.
Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omar Kipanga akaweka bayana mafanikio ndani ya sekta ya elimu kuwa katika kipindi cha miaka 20, chuo hicho kimefanikiwa kuwa na progrma zaidi ya 32 kutoka program mbili wakati kinaanza na kimefanikiwa kutoa wahitimu zaidi ya 15,000.
“Wahitimu hawa wamekuwa wwamekuwa wa kupigiwa mfano katika kazi na maadili inayofanya waaminiwe katika nafasi mbalimbali kwenye jamii na Serikali kaa ujumla”alisema.
Kadhalika, ameongeza kuwa Chuo hicho kimeweka mipango inayozingatia dira ya maendeleo ya Taifa ya 2050 na mwelekeo mpya wa Elimu Nchini Tanzania unaolenga kutoa Elimu Ujuzi, Stadi na Maarifa kwa ajili ya kuwajengea wahitimu uwezo na sifa za kujiajiri na kuajirika katika soko shindani la ajira duniani.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Waislamu (MDF),Dk Ramadhani Dau alisema Bodi na uongozi wa Chuo Kikuu hicho inamshuuru Rais wa Awamu ya Tatu , Benjamin William Mkapa kwa uamuzi wake wa kuwakambidhi majengo yaliyokuwa Chuo cha Tanesco mwaka 2005 ili kuanzisha chuo Kikuu hicho.
Naye Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir bin in Ali ametoa wito kwa Waislam na Watanzania kwa ujumla kuweka mikakati ya kukisaidia chuo ili kiendelee kufanya vizuri na kutoa elimu kwa watanzania nchini.
“Waislam na watanzania tukisaidie chuo hichi, hakuna uislam bila ualimu, uislam ulipokuja ulipiga sana vita ujinga, tuwaunge mkono viongozi wetu kwa kukisaidia chuo hiki”
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Mussa Assad alisema kuwa moja ya changamoto kubwa katika chuo hicho ni kukosekana kwa hosteli za wanafunzi wa kike.
"Namna tunavyoingeza udahili ndivyo tunavyoibua changamoto nyingine, tunataka watoto wetu wa kike wote wake ndani ya chuo,”alisema.
MWISHO.


No comments:
Post a Comment