![]() |
| Mkuu wa wilaya ya Longido, Salum Kalii akizindua mradi wa Maji katika Kijiji Cha Orkisma, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Monduli Festo Kiswaga |
![]() |
| Mkuu wa Wilaya ya Longido Salum Kalii akizungumza na wananchi wa Kijiji Cha Orkisma mara baada ya uzinduzi wa mradi wa maji |
| Wananchi wa Kijiji Cha Orkisma wakiimba na kufurahi mara baada ya kukabidhiwa mradi wa maji |
Mussa Juma,Monduli
maipacarusha@gmail.com
Shirika lisilo la kiserikali la FELOCI limezindua na kukabidhi kwa wananchi mradi wa maji wa kihistoria katika kitongoji cha Orkisima, kijiji cha Losimingori, wilayani Monduli, mkoa Arusha,mradi uliofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira duninia (GEF) kupitia programu za miradi midogo (SGP) inayoratibiwa na shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).
Mradi huo wa maji kwa zaidi ya miaka 20 ulikuwa umekwama licha ya miundombinu yake kujengwa wakati wa ukoloni mwaka 1959 kwa lengo la kusambaza maji katika vijiji mbalimbali katika wilaya hiyo.
Mradi huo umezinduliwa na Mkuu wa wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa wilaya ya Longido, Salum Kalii, katika hafla iliyofanyika katika kitongoji cha Orkisima na kuhudhuriwa na mamia ya watu ambao wanatarajia kunufaika na mradi huo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kalii alimpongeza Mkurugenzi wa FELOCI, ambaye pia ni Diwani wa kata hiyo ya Lepurko Yonas Laiser kwa kufanikisha mradi huo ambao utasaidia zaidi ya wananchi 6000 wa kijiji hicho.
"Huu ni mradi wa kihistoria tumeelezwa hapa wananchi walikuwa hawana maji kwa miaka 20 katika kijiji chao na hivyo kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata maji sasa maji ya watu na mifugo yamepatikana"alisema
Alisema kukamilika kwa mradi huo, pia kumechangiwa na jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama na ndio sababu mamlaka ya maji vijijini wilaya ya Monduli (RUWASA) imeshiriki kiasi kikubwa katika kufanikisha mradi huu ikiwepo kutoa utaalam.
"Tumpongeze pia Rais wetu Samia Suluhu kwa kufungua milango kwa mashirika ya kimataifa ikiwepo UNDP kufanyakazi nchini vizuri hadi kuweza kufadhili miradi hii ambayo inagusa maisha ya watu"alisema
![]() |
| Mkurugenzi wa FELOCI, Yonas Laizer akizungumza na wakazi wa Orkisma baada ya kukabidhi mradi wa maji |
Awali Mkurugenzi wa FELOCI, Yonas Laizer alisema katika utekelezaji wa mradi huo, wameweza kutandaza mabomba ya maji umbali ya kilomita 15 kutoka chanzo cha maji kilichopo katika msitu wa losimingori ambao unasimamia ya Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya wanyamapori nchini(TAWA) na kukarabati tanki kubwa la maji.
"Kazi haikuwa rahisi Mh mkuu wa wilaya, tulilala msituni kupandisha miundombinu na kufunga mabomba na tunashukuru sana maafisa wa TFS na TAWA kwa kutupa ushirikiano mkubwa na leo maji yamefika kijiji na tunakabidhi mradi"alisema
Alisema mradi huo ambao ni miongoni mwa miradi inayofadhiliwa na UNDP utaleta faraja kwa wananchi wa Kata nzima ya Lepurko kwani baadaye kuna mkakati wa kusambaza maji haya katika vijiji vingine kwani ni mengi sana.
"Zaidi ya lita 400,000 zinazalishwa kwa siku ni maji mengi na ndio sababu tutashirikiana na wadau kusambaza maji haya katika vijiji vingine kwani wananchi walikuwa wananunua ndoo moja ya maji hadi sh 500 na maji yalikuwa ya shida" alisema
Meneja wa RUWASA wilaya ya Monduli, Neville Msaki alisema Mamlaka hiyo, itaendeleza mradi huo kufika katika vijiji vingine kwani una manufaa makubwa kwa wananchi na maji yanapatikana ya kutosha.
"Tunampongeza sana Mkurugenzi wa FELOCI kwa kuja na mradi huu na tunawashukuru wafadhili UNDP, SGP na GEF kwa kuwezesha mradi huu ambao sasa tutausimamia pamoja na serikali ya kijiji kupitia kamati ya maji"alisema.
Wakizungumza katika makabidhiano hayo, baadhi wa wawakishi wa mashirika yanayofadhiliwa na UNDP kupitia programu hiyo ya miradi midogo, Shirika la MPDO-Lareto na Shirika la Wanahabari wa kusaidia jamii za asili (MAIPAC) walishukuru UNDP kwa ufadhili wa miradi ambayo inagusa maisha ya watu moja kwa moja.
Mkurugenzi wa MPDO-LARETO, Lebaraka Laiser aliwataka wananchi wa kitongoji cha Orkisima ,kijiji cha Losimingori kutunza mradi huo ili uwanufaishe kwa muda mrefu huku akiahidi shirika hilo kuendeleza mradi wa ujenzi wa madarasa katika kitongoji hicho cha Orkisima.
| Nyuso za furaha Toka kwa viongozi wa mashirika na Kijiji Cha Orkisma mara baada ya kukamilisha kazi ya kukabidhi mradi wa maji kwa wananchi |
MWISHO.



No comments:
Post a Comment