CUF YAWATAKA WATANZANIA KUTOKUWA WAOGA WA FIKRA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 23 October 2025

CUF YAWATAKA WATANZANIA KUTOKUWA WAOGA WA FIKRA

 




Na Lilian Kasenene,Morogoro

maipacarusha20@gmail.com 


Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito , amewataka  Watanzania kutokuwa waoga wa fikra ya kufanya mabadiliko na kuchukua hatua ifikapo Oktoba 29.


Hata hivyo mgombea huyo wa Urais aliwataka wananchi wajitokeze  kufanya mabadiliko kwenye sanduku la kura na kuwachagua wagombea wa chama hicho kwa nafasi ya  Urais, Wabunge na Madiwani.


Gombo alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Morogoro kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kituo cha zamani cha daladala mjini Morogoro na kubainisha kuogopa ama kuwa jasiri hakuzuii kufikwa na matatizo kama yakiamua kujitokeza.


Akawahimiza Watanzania kutumia kura zao Oktoba 29 kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi  na kwamba hata yeye kilichomsukuma kugombea nafasi hiyo ya Urais ni kutaka mabadiliko.


Akatolea mfano baadhi ya nchi za Afrika zilizofanya mabadiliko na bado uchumi wa watu wake umeendelea kuwa imara kuwa ni pamoja na Senegal, Malawi na Zambia hivyo kuwataka watanzania kubadilika kifikra na kukataa vitu kivitendo.


"Mnatakiwa kuua Tembo Kwa ubua, hamhitaji kutumia nguvu kubwa,nichagueni nishughulikie hizi changamoto lukuki ambazo zimeendelea kuwa mzigo kwa watanzania, mabadiliko hayahitaji miujiza,"alisema Samandito.


Mgombea huyo wa Urais pia aliahidi iwapo atachaguliwa , Serikali yake itahakikisha huduma za elimu na afya zinatolewa bure kwani fedha kwaajili hiyo zipo, watumishi wapya wanapatiwa viwanja na nyumba za makazi pindi wakianza Kazi.


Aidha akaahidi Wazee kulipwa posho kila mwezi, na Serikali kwani wametumikia nchi Kwa muda mrefu ,pamoja na kushughulikia kwa haraka changamoto za kikodi pamoja na  kutoa ajira kwa wote wenye sifa.


"Serikali yangu itaajiri watu wote wenye vyeti, lakini usichague pa kwenda, utakwenda eneo lolote lenye uhitaji na ukikataa cheti chako kitafutwa na hutapata ajira kokote kwingine hapa nchini "alisisitiza.


Kwa upande wake, Mgombea Ubunge kwa tiketi ya CUF Jimbo la Morogoro Mjini, Nyambi Rashid Athuman, aliahidi kutatua changamoto za jamii ikiwemo upatikanaji wa maji na elimu, kuwawajibisha viongozi na watumishi wa umma watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao, na kuanzisha Mfuko wa Rambirambi wa Jimbo.


Athuman alisema pia atahakikisha ujenzi wa bandari kavu unatekelezwa kwa ufanisi ili kuchochea uchumi wa wananchi wa Morogoro na mikoa jirani.


Mwisho.

No comments: