Na Lilian Kasenene, Dodoma
maipacarusha20@gmail.com
KATIKA kuhakikisha ubora wa taarifa zinazotolewa kwa umma unaongezeka,kuimarisha uwazi wa kifedha na kusaidia ukuaji wa uchumi kwa Waandishi wa Habari nchini,Banki kuu ya Tanzania(BoT) imeelwza kuwa itaendelea kutoa elimu ya uchumi na masoko ya fedha kwa wanahabari hao.
Meneja wa Huduma za Kibenki na Sarafu wa BoT Nolasco Maluli alisema hayo jijini Dodoma wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa Waandishi wa Habari kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Pwani, Morogoro na Zanzibar, yenye lengo la kuongeza uelewa na umahiri katika kuripoti masuala ya uchumi na fedha nchini.
Maluli alisema kuwa mafunzo hayo pia ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kuelewa kwa undani majukumu ya Benki Kuu, sera za fedha, mzunguko wa uchumi, usimamizi wa sekta ya fedha na namna taarifa sahihi za kifedha zinavyoweza kuchochea maendeleo.
"Mafunzo hayo yatachochea uwezo wa waandishi kufasiri takwimu na sera za fedha ili kutoa taarifa sahihi, wazi na zenye kuleta tija kwa umma ikiwa ni pamoja na kuwezesha kuelewa majukumu, muundo na taratibu za BoT,"alisema.
Aidha meneja huyo alisema anatarajia waandishi kujijenga na kuwa wenye weledi katika masuala ya uchumi, hususani kipindi ambacho taarifa sahihi za kifedha zina mchango mkubwa katika maamuzi ya sera, biashara na ustawi wa jamii.
Mafunzo haya pia yataimarisha mahusiano kati ya BoT na vyombo vya habari, kwa kuweka mazingira ya mawasiliano ya mara kwa mara ili kuongeza uwazi na upatikanaji wa taarifa sahihi.
Meneja Msaidizi wa Uchumi wa BoT Tawi la Dodoma, Shamy Chamicha, akitoa mada katika mafunzo hayo alieleza kwa kina muundo wa Taasisi hiyo na wajibu wake katika uchumi wa taifa kwa kueleza kuwa ina jukumu la kudhibiti na kusimamia sera ya fedha.
Chamicha alisema ili kuhakikisha thamani ya shilingi inabaki na kuwa thabiti na mfumuko wa bei unakuwa katika kiwango kinachokubalika Waandishi wa Habari Wana wajibu wa kuhabarisha jamii.
Chamicha alisema kuwa sera ya fedha ndiyo injini inayowezesha uchumi kukua kwa kasi bila kujenga misukosuko ya kiuchumi.
"BoT ina jukumu la kusimamia mfumo wa kifedha, ikiwemo utoaji wa leseni kwa mabenki, usimamizi wa taasisi za fedha, ufuatiliaji wa mifumo ya malipo na kuhakikisha usalama wa amana za wananchi,uthabiti wa sekta ya fedha ni msingi muhimu wa uchumi imara,"alisema.
Aidha Chamicha alifafanua kuwa Benki Kuu pia inahusika katika kusimamia na kudhibiti usambazaji wa sarafu nchini, kuhakikisha inatosheleza mahitaji ya wananchi, ni halali, salama na yenye ubora.
Alisema BoT inaendelea kufanya maboresho ya mifumo ya malipo ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kuunga mkono ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Meneja huyo msaidiI alizungumzia mfumo wa utekelezaji wa Sera ya Fedha unaotumia riba na faida zake, napo alisema BoT hutumia mfumo huo kudhibiti mzunguko wa fedha kwenye uchumi ili kuhakikisha bei za bidhaa na huduma zinabaki katika viwango vinavyokubalika.
"Riba ni chombo muhimu katika kusimamia mwenendo wa uchumi kwa kuwa inapoongezwa, upunguza kasi ya mikopo na matumizi, jambo linalosaidia kupunguza mfumuko wa bei,"alisema.
Alisema kuwa BoT hufanya tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha mabenki yanatoa huduma kwa viwango vinavyowezesha uchumi kukua bila kuhatarisha uimara wa sekta ya fedha.
"Huu mfumo wa sera ya fedha unaohusisha riba husaidia kupunguza hatari za kiuchumi, kuongeza uwazi katika soko la fedha na kuweka mazingira salama ya upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara na sekta binafsi,".
Mwisho.

No comments:
Post a Comment