Na Mwandishi wetu, Kiteto
maipacarusha20@gmail.com
DIWANI wa Kata ya Dosidosi Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, Hamza Ally Mngia amejitosa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mngia ambaye ni mara yake ya kwanza kushinda nafasi ya udiwani akizungumza wakati akirejesha fomu ya kugombea amesema yeye bado ni kijana anayeamini uwezo, bidii na ufanisi wa kutumikia nafasi hiyo ya Mwenyekiti pindi akichaguliwa.
"Wakati huu Mwenyekiti wa CCM na Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameonesha wazi kutuamini vijana na kutupa nafasi kubwa mbalimbali za kimaanuzi nchini na hiyo ndiyo sababu iliyonipa nguvu ya kuiomba nafasi hii ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya kiteto," amesema.
Amesema kwa sasa ni kusubiri mchakato na utaratibu wa vikao vya chama na hana hofu na CCM kwani anayo imani kubwa ukilinganisha na sifa zake za kiuongozi alizonazo.
"Nikifanikiwa kuteuliwa nikianza kampeni nitaeleza sababu zangu kwanini nimegombea nafasi hii na nataka kufanya nini kwa maslahi mapana ya wana Kiteto," amesema Mngia.
Mngia anapambana na wagombea wengine madiwani wenzake saba akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Abdalah Bundala, Diwani wa Kata ya Songambele.
Wagombea wengine wa nafasi hiyo ni Lameck Kaila (Chapakazi), Christopher Parmet (Kaloleni), Said Ndiboy (Matui), Bahati Mliuka (Bwawani) na Sokoine Ortus (Loolera).
MWISHO

No comments:
Post a Comment