MISA TAN YATAKA HABARI ZA KUPONYA MAJERAHA YA OCTOBER 29 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 27 November 2025

MISA TAN YATAKA HABARI ZA KUPONYA MAJERAHA YA OCTOBER 29

 


Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko

Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Naibu kamishna wa Polisi David Msime akiwasilisha mada kwa waandishi wa Habari
Na Mwandishi Wetu, Maipac 

maipacarusha20@gmail.com 


Taasisi ya waandishi wa habari kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (Misa- Tan) imewataka Waandishi wa habari nchini kuandika habari za kuiponya jamii kutokana na matukio ya mauaji na vurugu  za October 29 na 30 .

Mwenyekiti wa Misa Tan  Edwin Soko ameyasema hayo wakati akizungumza  katika  mafunzo maalumu ya Uandishi wa habari wa Amani (Peace Journalism) katika programu iliyowakutanisha waandishi 100 kutoka mikoa yote nchini ili kuwaongezea ujuzi na mbinu za kuandika na kuripoti habari zinazolinda na kuimarisha amani ya taifa.


Katika Mafunzo hayo ya siku moja yakiongozwa na kauli mbiu 'Empowering Journalists to build peace through ethical reporting' yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), yamefanyika leo Novemba 27, 2025 jijini Dodoma,Soko alisema kilichotokea October 29 na 30 kimeliumiza taifa.

Amesema kwa Sasa wanahabari  wanapaswa kuandika habari za kuhimiza Amani na kuliondoa taifa katika madhila yaliyojitokeza.

"Tuandike habari za Amani tuache kuchochea moto,tuandike habari za kusaka Suluhu na kutorokea tena katika vurugu"alisema

 Alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waandishi kuelewa dhana ya Uandishi wa Habari wa Amani, aina mpya ya uandishi wa habari unaojikita katika kuimarisha utulivu, kuzuia uchochezi, kupunguza upotoshaji, na kuripoti habari kwa namna inayojenga maelewano na mshikamano katika jamii.

Amesema waandishi wa habari ni daraja muhimu linalounganisha Serikali na wananchi, hivyo lazima watekeleze wajibu wao kwa uadilifu bila kuyumbishwa na mtu yeyote mwenye nia ya kuichafua tasnia ya Habari.

“Vyombo vya habari ni nguzo kubwa ya usalama wa Taifa,” amesema Soko.

 “Hatutaruhusu mtu yeyote kutikisa au kuathiri misingi yetu ya uzalendo. Waandishi wa Tanzania ni wazalendo, si wasaliti”,ameeleza Soko.

Akigusia tukio la Oktoba 29, Soko amesema sekta ya habari iliguswa moja kwa moja, kwani baadhi ya waandishi waliumia, walipoteza wenzao na wengine kupoteza vifaa vya kazi.

Ametoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Ndani kuendelea kulinda amani ya nchi pamoja na kuhakikisha waandishi wanakuwa salama wanapotekeleza majukumu yao.

Ameongeza kuwa MISA Tanzania itaendelea kutoa mafunzo ya Uandishi wa Habari wa Amani ili kujenga uwezo wa wanahabari kuandika habari zinazohamasisha amani, kushusha joto la mgogoro, kupunguza taarifa za uchochezi na kuongeza umoja wa kitaifa.


 Akifungua mafunzo hayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Denis Lazaro Londo, amesema waandishi wa habari wana jukumu muhimu la kulinda umoja wa kitaifa kupitia matumizi ya lugha inayojenga, utoaji wa taarifa sahihi, na kuepuka taarifa zinazoweza kuchochea au kusababisha migogoro, hasa katika vipindi nyeti kama vile chaguzi na migogoro ya kijamii.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Denis Lazaro Londo.


Amesema mafunzo hayo yametolewa katika kipindi sahihi, baada ya tukio la Oktoba 29, ambapo taifa kwa sasa linahitaji habari sahihi, zenye utulivu na zinazolinda ustawi wa nchi.

“MISA Tanzania ni mdau mwaminifu kwa Serikali hata katika nyakati ngumu tulizozipitia. Huo ndiyo uzalendo tunaoutaka kwa maslahi ya taifa,” amesema Londo.

Ameongeza kuwa Wizara yake itaendelea kulinda usalama wa waandishi wa habari na vifaa vyao wanapotekeleza majukumu yao, sambamba na kupongeza vyombo vya habari kwa kutoa taarifa nyingi za kutetea na kuhimiza amani kupitia viongozi wa dini na Jeshi la Polisi.



 Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenedy Simbaya, ameishukuru MISA Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo, akibainisha kuwa ni chachu muhimu ya kuimarisha umoja, mshikamano na maelewano ndani ya taifa.



Mwenyekiti wa chama Cha wafanyakazi katika vyombo vya habari (JOWUTA) Mussa Juma akizungumza katika mkutano huko alisema waandishi wa habari nchini hawataki yatokee Tena matukio ya vifo kama ilivyokuwa October 29 na 30 mwaka huu.
 


Juma alisema waandishi wa habari wamekuwa pia wahanga wa vurugu kwani waandishi watatuma waliuwa kwa risasi.

"Mheshimiwa mgeni rasmi sisi kama wanahabari tusingependa mauwaji yaliyotokea kujirudia ndiyo sababu tunataka Suluhu kupatikana"alisema

Alisema JOWUTA itaunga mkono jitihada zozote za kuhakikisha Amani ya kudumu inarejea nchini ili kutoathiri Maisha na uchumi wa watu.

Akiwasilisha mada katika Mafunzo hayo msemaji w jeshi la Polisi Nchini kamishna msaidizi wa Polisi David Msime amesema kuwa wanahabari Wana mchango mkubwa wa kuimarisha Amani ya Nchi kwa kuandika habari chanya zenye mlengo wa kujenga Amani ya Nchi.

Mwisho.


No comments: