Ongezeko la joto dunia kilio COP 30,mikakati yawekwa. .Jitihada za wadau UNDP, Jamii za asili na Azaki zatajwa - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 14 November 2025

Ongezeko la joto dunia kilio COP 30,mikakati yawekwa. .Jitihada za wadau UNDP, Jamii za asili na Azaki zatajwa



Martha Fatael,Maipac

maipacarusha@gmail.com


Wakati viongozi wa Dunia wanakutana jijini Belém nchini Brazil, kwa ajili ya Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP30), wito wa kasi na utekelezaji umepewa kipaumbele hasa kukabiliana na ongezeko la joto duniani.


Ongezeko hili la joto ni moja za athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayotokana na uharibifu wa mazingira.


Katibu Mtendaji wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa, Simon Stiell, amesisitiza kuwa sasa ni wakati wa kuchukua hatua na si maneno katika kudhibiti ongezeko la joto duniani hadi chini ya nyuzi joto 1.5.


Stiell amebainisha hayo wakati akifungua mkutano huo kwa kauli isemayo “ _Dunia haina tena muda wa kupoteza,”_ huku akisisitiza kuwa si wakati wa maneno bali wakuchukua hatua.


Kauli hiyo imeonekana kama onyo kwa mataifa yaliyosaini Makubaliano ya Paris ya mwaka 2015, mkataba wa kimataifa unaolenga kudhibiti ongezeko la joto duniani hadi chini ya nyuzi joto 1.5, lakini yameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.


*Wito wa dharura kutoka Umoja wa Mataifa*

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Katika hotuba yake ya ufunguzi iliyotolewa Novemba 6, 2025, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, ameonya kwamba Dunia iko hatarini kupoteza dira ya kudhibiti ongezeko la joto duniani.


“Ukweli mchungu ni kwamba tumeshindwa kuhakikisha Dunia inabaki chini ya nyuzi joto 1.5. Hata ongezeko dogo la muda litakuwa na madhara makubwa na linaweza kusukuma mifumo ya ikolojia kuvuka mipaka isiyoweza kurekebishwa, kuwaweka mabilioni katika hali zisizoishiwa, kuongeza vitisho kwa amani na usalama,” amesema Guterres.


Kauli hiyo ilitafsiriwa kama wito wa dharura wa kisayansi na kisiasa, kwamba kila taifa linapaswa kuongeza kasi ya utekelezaji wa ahadi zake za Nationally Determined Contributions (NDCs), yaani michango ya kitaifa iliyokusudiwa kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kuachana na utegemezi wa nishati ya kisukuku kwa vitendo, si kwa mikataba pekee.


Utekelezaji uliosubiriwa kwa muda mrefu


Kauli za Guterres na Stiell zinakuja wiki chache baada ya wataalamu wa mazingira nchini Tanzania kutoa wito kama huo, wakisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa ahadi zilizotolewa katika vikao vya COP vilivyopita.


Ofisa Mazingira Mwandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt.Makuru Nyarobi, amesema tatizo kubwa si makubaliano bali utekelezaji wake.


“Sisi tunaona mataifa makubwa yana wajibu wa kufanya, maana yamechangia zaidi katika uzalishaji wa gesijoto. Wasiwasi ni pale ambapo hatufikii makubaliano kwa sababu kila taifa linakuja na matarajio yake, lakini ukweli ni kwamba hatuwezi kuwajibika sawa kwa sababu hatukuharibu sawa,” amesema Dkt. Nyarobi.


Ameongeza kuwa kuchelewesha utekelezaji kunamaanisha gharama kubwa zaidi kwa mazingira, hasa kwa nchi kama Tanzania, ambako athari zimeanza kuonekana wazi kupitia kuyeyuka kwa barafu ya Mlima Kilimanjaro.


*Athari za kuyeyuka kwa barafu ya mlima Kilimanjaro*


Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam (UDSM), zaidi ya asilimia 80 ya barafu ya Kilimanjaro imeshayeyuka ndani ya karne moja.
 Mabadiliko haya yameathiri moja kwa moja vyanzo vya maji, kilimo, na maisha ya jamii katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.


Mtafiti wa mabadiliko ya tabianchi kutoka UDSM, Profesa Pius Yanda, amesema kuyeyuka kwa barafu la Kilimanjaro si jambo la kijiografia pekee, bali ni ishara ya mfumo wa ikolojia unaoporomoka.


“Tukipoteza barafu hizi, tunapoteza chanzo muhimu cha maji, urithi wa Dunia na utalii unaotegemewa na maelfu ya watu,” amesema Profesa Yanda.


Kwa upande wake, Profesa Margaret Lema wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema kuyeyuka kwa barafu ni kiashiria cha kuvurugika kwa mifumo ya ikolojia ya milimani na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa katika ukanda wa tropiki.


Mtaalamu mwingine wa mazingira, Dkt. Elibariki Mushi, amebainisha kuwa Tanzania inapaswa kutumia fursa ya COP30 kutafuta fedha kupitia Green Climate Fund (GCF) kwa ajili ya miradi ya uhimilivu wa milima na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Watu wa jamii za asili walivuobamia COP 30 

*Kasi ndogo ya utekelezaji wa Paris na NDC*


Kwa mujibu wa ripoti mpya ya NDC Synthesis, Dunia imeanza kuona dalili za mafanikio katika kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwa mara ya kwanza tangu kipindi cha mageuzi ya viwanda, kiwango cha gesi joto kimeanza kupungua.


Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa, Simon Stiell ameonya kuwa mafanikio hayo bado ni madogo,


“Kila sehemu ndogo ya nyuzi joto tunayoepuka ni maisha, chakula na usalama tunaouokoa. Lakini kasi tuliyonayo sasa haitoshi,”amesema Stiell.


Akizungumza Mto Amazon, Stiell ametumia mfano wa mfumo wa mito inayounganika kuwa Mto Amazon hauitegemei chanzo kimoja cha maji kama ambavyo COP haiwezi kutegemea taifa moja pekee hivyo Dunia nzima lazima iwe sehemu ya mkondo wa utekelezaji.


Kauli hiyo inalingana moja kwa moja na hali ya Mlima Kilimanjaro ambao unatiririsha maji yake kuelekea mabonde yanayolisha mamilioni ya watu, hivyo ikiwa Dunia itashindwa kushikamana, maji hayo yanaweza kubaki kuwa historia.


*
Wito kwa Tanzania*


Mshauri wa Rais katika masuala ya tabianchi, Dkt. Salim Njoroge, amesema Serikali inapaswa kutumia jukwaa la COP30 kuwasilisha hoja ya kuanzishwa kwa kipengele cha fidia ya kimazingira kwa nchi zinazopoteza urithi wa asili kutokana na mabadiliko ya tabianchi.


Kwa upande wake Mkuu wa Sekta ya Sayansi Asilia wa UNESCO, Keven Robert, amesema mwaka huu wa 2025 unatoa fursa kwa Tanzania kuonesha uongozi wake wa kimazingira kupitia urithi wa Mlima Kilimanjaro, ambao ni alama ya maisha na ukumbusho wa gharama ya uzembe wa Dunia.


Wadadisi wa masuala ya kidiplomasia na mazingira wamechukulia kauli za Stiell na Guterres kuwa si hotuba za kidiplomasia pekee, bali ni kilio cha sayansi, uchumi na uhai wa dunia.


Mmoja wa wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam es Salaam (ambaye hakutaka kutajwa kwa jina), amesema kazi ya utekelezaji itapimwa si kwa maneno bali kwa theluji tutakayoona imebaki kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro miaka 10 ijayo.


*Jitihada za Asasi za Kiraia na ufadhili wa UNDP*

Baadhi ya watendaji wa asasi za kiraia nchini ambao walipokea ufadhili wa miradi UNDP ,wakiwa na watendaji wa shirika la UNDP Tanzania

Asasi kadhaa za kiraia nchini zimekuwa na jitihada kubwa za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi lakini pia kuzuia uharibifu zaidi wa mazingira.


Miongoni mwa asasi hizo ni taasisi ya wanahabari ya usaidizi jamii za pembezoni (MAIPAC) kupitia programu ya miradi midogo (SGP) inayodhaminiwa na Mfuko wa mazingira duniani kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).


Mussa Juma ni Mkurugenzi wa Shirika hilo anasema wamekuwa na mradi wa kukusanya maarifa ya asali katika uhifadhi wa mazingira ,vyanzo vya maji na misitu ili yaweze kutambulika na kutumika sasa na watungaji wa sera.


"Katika mradi huu tunakusanya maarifa ya asili katika uhifadhi kwa jamii za kimasai, hadzabe na Datoga ili kuona zinaweza kutumika sasa katika uhifadhi kwa kuunganisha na technolojia za kisasa"alisema.


Juma anasema jamii za asili zina maarifa ambayo yakitumiwa sasa yanaweza kusaidia jitihada za kuokoa dunia kutokana na ongezeko la joto duniani.


"Tunashukuru UNDP kwa miradi ambayo tunaendelea nayo sisi na mashirika mengine zaidi ya 20 hapa nchini katika kukabiliana na suala la mabadiliko ya tabia nchi lakini kuwezesha jamii kupunguza uharibifu wa mazingira na kuwa himilivu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi"amesema.


Mwisho


 



No comments: