TAWA na Mwiba Wajenga zahanati ,madarasa na Ofisi za walimu Meatu - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 26 November 2025

TAWA na Mwiba Wajenga zahanati ,madarasa na Ofisi za walimu Meatu





Mwandishi Wetu, Meatu


Wananchi wa Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, wanatarajiwa kuondokana na changamoto za upatikanaji wa huduma za afya na elimu baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kwa kushirikiana na Kampuni ya Kitalii ya Mwiba Holdings Ltd., kuanzisha miradi ya ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Matale pamoja na madarasa manne na ofisi mbili za walimu katika Kijiji cha Mbugayabanya.


Miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia TAWA na Mwiba Holdings Ltd. katika kuboresha huduma za jamii na kuhakikisha wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi wananufaika na rasilimali za wanyamapori.


Akizungumza jana katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika vijiji hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Fauzia Ngatumbura, aliipongeza TAWA na Mwiba Holdings Ltd. kwa kuibua miradi yenye manufaa makubwa na inayogusa mahitaji halisi ya wananchi. Alitoa rai kwa wananchi kuilinda miradi hiyo na kuendelea kuthamini jitihada za wadau wa uhifadhi.


“Niwapongeze sana TAWA kwa kushirikiana na wadau wenu kwa kusimamia vizuri miradi hii. Mmefanya kazi kubwa kwa kuibua miradi kulingana na mahitaji ya kila kijiji," alisema Ngatumbura.


Aliongeza kuwa, “Wito wangu kwenu wananchi ni kuendeleza ushirikiano katika kulinda hifadhi zetu, kwani kupitia rasilimali hizi tunaweza kupata fedha za kigeni na kufanikisha miradi mingi zaidi."


Ujenzi wa zahanati hiyo, ambayo umefikia asilimia 63, unatarajiwa kupunguza adha ya akina mama na watoto wanaotembea umbali mrefu kufuata huduma za afya. Wakati huohuo, ujenzi wa madarasa manne na ofisi mbili za walimu, uliokamilika kwa asilimia 75, unatarajiwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.


Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo inayofadhiliwa kupitia shughuli za uhifadhi na utalii chini ya mpango wa Uwekezaji Mahiri (SWICA) katika Pori la Akiba la Maswa, Afisa Uhifadhi wa TAWA Kanda ya Ziwa, Lusato Masinde, alisema ujenzi wa zahanati hiyo utagharimu zaidi ya Sh milioni 286 na ujenzi wa madarasa na ofisi za walimu utagharimu Sh milioni 216.7.


Alisema Miradi yote imeanza kutekelezwa Oktoba 25, 2025 na inatarajiwa kukamilika Desemba 2025.


Masinde alisema TAWA itasimamia kikamilifu miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa


Baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa na miradi hiyo, wakisema imekuja wakati muafaka na kuongeza imani kwa Serikali.


Jeremiah Masunga alipongeza Mwiba na TAWA kwa kuendelea na miradi ya kuboresha maisha yao ambayo ni faida ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira.


Alisema Wilaya ya Meatu inapiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za kijamii .


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi ya Jamii wa Mwiba Holdings Ltd., Aurelia Mtui, alisema kampuni hiyo imekuwa ikiunga mkono jamii kupitia miradi ya elimu, afya, na uhifadhi. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na chakula cha bure kwa wanafunzi, usafiri kwa wanafunzi wanaoishi mbali na shule, ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, na nyumba za wahudumu wa afya.


"Tumekuwa pia tukifadhili masomo ngazi ya vyuo kwa watoto kutoka kaya masikini, tumefunga kola tembo katika mradi wa utafiti ili kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyama, na kutoa mafunzo ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu,” alisema Mtui.


Aliongeza kuwa kwa sasa wanaendelea kugharamia matibabu ya watoto wenye ulemavu unaotibika kama midomo sungura, ulemavu wa miguu (matege, miguu vifundo) pamoja na majeraha yanayotibika, bila kusahau kutoa elimu muhimu ya uhifadhi wa mazingira na ujasiriamali ili jamii iweze kujikwamua.


Mwisho







No comments: