![]() |
| Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Ashatu Kijaji |

![]() |
Mwandishi wetu, Dodoma
maipacarusha20@gmail.com
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Ashatu Kijaji (Mb), amewataka watumishi wa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuhakikisha wanazingatia maslahi na utu wa Mtanzania wanapotoa huduma kwa wananchi lakini pia kuhakikisha watalii wanaongezeka nchini.
Dk. Kijaji ameyasema hayo jijini Dodoma mara baada ya kuripoti kazini na kufanya mazungumzo na menejimenti ya wizara, baada ya kuapishwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Amesema ni muhimu watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia utu na maslahi ya wananchi ili kuhakikisha wanapata huduma bora na maendeleo wanayostahili.
“Wananchi wanatuhitaji kwa yale tuliyoaminiwa kuyatekeleza kwa niaba ya Watanzania milioni 61. Ni jukumu letu kuwawezesha ili waendelee kuishi vizuri kama kawaida,” amesema Dk. Kijaji
Amefafanua kuwa Ilani ya CCM imeweka mkazo katika ustawi wa watu, na ustawi huo hauwezi kupatikana endapo changamoto kama wanyamapori waharibifu hazitatatuliwa.
“Mkulima amelima ekari 20 za mbaazi, zimekomaa, halafu zinaharibiwa na tembo, ustawi haupo hapo. Hivyo lazima tufikirie mbali ili kulinda ustawi wao,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa falsafa ya Kazi na Utu ya Mhe. Rais inahitaji mtumishi kumweka mwananchi mbele: “unapomhudumia mtu, jiulize ungependa kuhudumiwa vivyo hivyo? Huo ndio msingi wa kazi yetu.” amesema Dk. Kijaji
Waziri Kijaji pia ametoa wito kwa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na mshikamano ili kutimiza ndoto Watanzania kuongeza mapato kupitia sekta za uhifadhi, maliasili na utalii.
Waziri pia amewapongeza kwa kazi wanayoifanya na kuhimiza kuendeleza ushirikiano ili kufikia malengo ya wizara.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mhe. Hamad Hassan Chande ameishukuru menejimenti na watumishi kwa mapokezi mazuri na kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kuzingatia utu.
“Tumekuja kuungana nanyi katika ujenzi wa taifa. Hatukuja kama watawala, bali kama viongozi wa kutimiza ndoto ya Rais fanyeni kazi kwa utu, na mtambue thamani ya watu,” amesema Mhe. Chande
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Hassan Abbas, ameahidi kutoa ushirikiano kwa uongozi mpya ili kufanikisha malengo ya wizara na serikali, hususan katika kuhudumia wananchi na kutangaza vivutio vya utalii.
Awali, Waziri Dk. Kijaji alikagua gwaride maalum lililoandaliwa na Jeshi la Uhifadhi (JU) akiongozwa na Katibu Mkuu, Dk. Abbas.
Hata hivyo katika utekelezaji majukumu ya Wizara hiyo miongoni mwa changamoto ambazo zinatarajiwa kupatiwa ufumbuzi ni migogoro katika maeneo ya hifadhi za jamii za wanyamapori nchini(WMA) baina ya viongozi wa WMA hizo,Wawekezaji na Wananchi.
Mhifadhi Joram Mallya akizungumza na MAIPAC alishauri wizara kuja na mkakati mpya wa usimamizi wa WMAs ili kuhakikisha wanapatikana viongozi wenye sifa na uwezo wa kuziendesha.
"Miongoni mwa maeneo muhimu ya uhifadhi ni WMAs lakini hadi.sasa naweza kusema WMAs moja tu ya IKona tu kati ya WMAs 38 ndio inafanya vizuri na changamoto kubwa na uongozi kushindwa kutimiza majukumu ya kuziendesha lakini kwendana na mahitaji ya serikali kuongeza vivutio vya utalii na kumaliza migogoro katika maeneo hayo"alisema
Mallya pia alieleza Wizara bado inapaswa kukabiliana na changamoto ya uvamizi maeneo ya mapito ya wanyamapori(Corridol) hatua ambayo inachangia kuongezeka migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu.
Mwisho




No comments:
Post a Comment