WAZIRI KIJAJI: Ataka Utalii Jumuishi, Aipongeza TANAPA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 28 November 2025

WAZIRI KIJAJI: Ataka Utalii Jumuishi, Aipongeza TANAPA


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji


Mwandishi wetu, Maipac

maipacarusha20@gmail.com 


Arusha.Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), ameagiza uwepo wa utalii na uhifadhi jumuishi kwa kuwashirikisha wananchi katika ulinzi wa rasilimali za Taifa.


Akizungumza katika ziara yake ya kutembelea Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) jijini Arusha katika ziara maalum iliyolenga kufuatilia na kujifunza shughuli za Utalii na Uhifadhi alisema wananchi wanapaswa kuwa mbele katika kuzilinda na kuzitunza rasilimali za nchi kwa manufaa ya sasa na kizazi cha baadae.


Waziri Kijaji alisema "Uhifadhi ni msingi wa uhai, uchumi, utalii na ni fahari ya Taifa letu hivyo ni lazima jitihada za uhifadhi ziimarishwe.

"Tunahimizana sisi Tanzania kuwa namba moja katika utalii Afrika na duniani, tuna kila sababu ya kuwa namba moja ndani ya Afrika na dunia" alisema

Waziri Kijaji aliielekeza Menejimenti ya TANAPA kuendelea kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wageni wanaozitembelea Hifadhi za Taifa pamoja na ulinzi wa rasilimali za Taifa.


Alisema ni lazima kufikiwa lengo la Serikali la kupokea watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.


" Hivyo Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwemo TANAPA mnajukumu la kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa"alisema


Alisema Serikali pia imepanga kuongeza idadi ya askari, vituo, vifaa na matumizi ya teknolojia hivyo tuvitumie vizuri katika kutekeleza majukumu yenu.


"Tuwe na ubunifu wa vivutio vipya kwenye maeneo yetu ambavyo vitasaidia kufika lengo la kuongeza mapato , pamoja na kuongeza nguvu ya kuvitangaza "alisema


Awali Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande (Mb) alisema uhifadhi ni heshima ya nchi na dhamana ya kuulinda imekabidhiwa kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu, hivyo wana wajibu wa kuwajibika masaa 24 .


Naibu Waziri Chande amehimiza kuendelea kuifanyia maboresho miundombinu ya hifadhini ili iwe rafiki kwa watalii ili kurahisisha shughuli za kitalii bila kupata changamoto yoyote.


Kwa upande wake, Kamishana wa Uhifadhi TANAPA, Mussa Nassoro Kuji, alisema ujio wa Waziri ni chachu ya kuimarisha juhudi za uhifadhi maliasili katika Hifadhi za Taifa.


Kuji ambaye amefanya mapinduzi makubwa ya utendaji na uhifadhi TANAPA alibainisha kuwa TANAPA itaendelea kulinda bioanuai, kuboresha mifumo ya ulinzi wa wanyamapori na kusimamia rasilimali za hifadhi kwa kutumia teknolojia na mbinu za kisasa.


Waziri Dk Kijaji katika ziara hiyo aliambatana na Katibu mkuu wa wizara hiyo Dk Hassan Abbas na watendaji wengine wa wizara hiyo.



No comments: