COCA-COLA KWANZA, ORYX GAS TANZANIA YAZINDUA SOKO LA CHAKULA MSAMVU STAND KUCHOCHEA MATUMIZI YA NISHATI SAFI. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 19 December 2025

COCA-COLA KWANZA, ORYX GAS TANZANIA YAZINDUA SOKO LA CHAKULA MSAMVU STAND KUCHOCHEA MATUMIZI YA NISHATI SAFI.

 





Na Lilian Kasenene,Morogoro



maipacarusha20@gmail.com


WANAWAKE zaidi ya 450 waliopo kwenye biashara ya mama lishe mkoa wa Morogoro wanatarajiwa kufikiwa kupitia Mradi wa Mwanamke Shujaa unaoendeshwa na Coca-Cola Kwanza kwa kushirikiana na Oryx Gas Tanzania.


Katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kupitia mradi huo mama lishe 150 wa eneo la Msamvu tayari wamefikiwa.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa mawasiliaano ya jamii Coca-Cola Kwanza, Salumu Nasoro alisema kuwa mradi huo unalenga kuwaokoa wanawake wanaojishughulisha na biashara ya mama lishe dhidi ya athari za kiafya na kimazingira zitokanazo na matumizi ya kuni na mkaa katika maeneo yao ya kazi.


Juhudi za kukabiliana na changamoto za matumizi ya nishati chafu, uharibifu wa mazingira na magonjwa yatokanayo na moshi wa kuni na mkaa zimepata msukumo mpya kufuatia uzinduzi wa Soko la Chakula la Stendi ya Msamvu, lililoanzishwa chini ya Mradi wa Mwanamke Shujaa.


Nasoro alisema kuwa kwa Mkoa wa Morogoro, wanufaika wa mradi ni wanawake 450, huku wanawake 150 wakitoka katika eneo la Msamvu pekee.


Alifafanua kuwa mradi huo umejikita katika kuwawezesha wanawake kiuchumi na kiafya kwa kuwapatia mazingira salama na rafiki kwa mazingira ya kuendeshea shughuli zao za ujasiriamali.


“Mradi wa Mwanamke Shujaa unaweka mkazo katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususani gesi ya LPG, ili kupunguza magonjwa ya njia ya hewa, kulinda mazingira na kuongeza tija kwa wanawake wafanyabiashara,” alisema Nasoro.


Kupitia mradi huo, soko maalum la Msamvu limeanzishwa likiwa na vibanda 50 vya kisasa, vilivyopangika na salama, hatua inayowaondoa wanawake waliokuwa wakifanya biashara katika mazingira hatarishi kando ya barabara na maeneo yasiyo rasmi.


Aidha, mradi huo unatekeleza malengo yake kupitia mafunzo ya ujasiriamali na uendeshaji wa biashara, kuongeza fursa za kipato na ajira kwa wanawake pamoja na kuwapatia vitendea kazi vya kisasa na mazingira bora ya kufanyia kazi


Balozi wa Nishati Safi Jenepha Mosha alisema matumizi ya gesi ya kupikia yanachangia kukuza uchumi wa kaya, kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji miti, na kulinda afya ya wanawake ambao ndio waathirika wakubwa wa moshi unaotokana na kuni na mkaa.


“Nishati safi ni suluhisho la moja kwa moja la changamoto za kiafya na kimazingira. Wanawake wanapobadili mtindo wa kupikia, tunapunguza hewa chafu, tunahifadhi misitu na tunaboresha maisha,”alisema Mosha.


Katika kuunga mkono jitihada hizo, Oryx Gas Tanzania imetoa mitungi ya gesi yenye thamani ya shilingi milioni 11, hatua inayorahisisha upatikanaji wa nishati safi kwa wanawake wanufaika wa mradi huo.


Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Mkuu wa Idara ya Viwanda na Biashara, John Kulunge alisema Manispaa imeingia ubia na wadau wa maendeleo ili kutatua changamoto ya matumizi ya nishati chafu ya kupikia, akisisitiza kuwa nishati safi ni ajenda ya kitaifa.


“Matumizi ya nishati safi ni kipaumbele cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan kupitia nishati safi, tunaokoa misitu na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa,” alisema Kulunge.


Aliongeza kuwa mafunzo yaliyotolewa yameleta mabadiliko ya mtazamo kwa wanawake wanufaika, hasa baada ya kukabidhiwa vitendea kazi vya kisasa vinavyowezesha ufanisi na usalama katika biashara zao.


Meya wa Manispaa ya Morogoro, Khalid Matengo aliwataka wafanyabiashara wa chakula (mama lishe) katika eneo la Msamvu kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa kuanzisha vikundi vya kijamii na kiuchumi.


Uzinduzi wa soko hilo unaonesha dhamira ya Coca-Cola Kwanza na wadau wake katika kuunga mkono maendeleo endelevu, kuboresha maisha ya jamii na kuchangia ajenda ya taifa ya matumizi ya nishati safi, ulinzi wa mazingira na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.


Kupitia mradi huu, soko maalum Msamvu limeanzishwa likiwa na vibanda 50 vya kisasa, salama na vilivyopangika, kusaidia wanawake waliokuwa wakifanya biashara katika mazingira magumu barabarani.



Coca-Cola Kwanza inasisitiza dhamira yake ya kuunga mkono jamii, kuboresha maisha na kuleta maendeleo shirikishi kwa manufaa ya jamii na biashara.


Mwisho.

No comments: