Na Mwandishi wetu, Simanjiro
maipacarusha@gmail.com
DIWANI wa Kata ya Komolo, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Saning'o Kipoon Somi (Dokta wa mipaka) ameeleza kwamba ameongoza kwa uadifu nafasi Mwenyekiti wa Kijiji cha Komolo kwa miaka 10 ndiyo sababu akachaguliwa kuongoza kata hiyo.
Saning'o ameyasema hayo kwenye sherehe na misa ya shukrani kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo na kumuomba Mungu ampe kibali cha kuongoza Komolo.
Saning'o ameeleza kwamba katika uongozi wake wa miaka 10 hakukuwa na mgogoro wa ardhi wa mtu na mtu ndiyo sababu akapewa jina la daktari wa mipaka.
"Kwa kipindi changu cha miaka 10 niliyoongoza na kuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Komolo, hakukuwa na kesi ya kugombea ardhi kati ya mtu na mtu hadi nilipokabidhi kijiti kwa Mwenyekiti mwingine," amesema Saning'o.
Ameeleza kwamba hata uongozi uliopo hivi sasa alipowakabidhi ofisi aliacha nyaraka ya kila jambo la ardhi hivyo ana uhakika wataendelea vyema pale alipoachia.
Padri kiongozi wa Kanisa Katoliki mission ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili Terrat, Edwin Kiromo amemsihi Saning'o kumtanguliza Mungu katika uongozi wake akiwatumikia watu wa Komolo.
"Tenda wema, patanisha watu, peleka furaha kwa watu, usiwe na hila, omba hekima kama Suleiman hakuomba mali wala ng'ombe kwa Mungu, aliomba hekima akapewa na mali zaidi katika uongozi wake," amesema Padri Kiromo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima amempongeza Saning'o kwa kushika nafasi hiyo baada ya kuchaguliwa na wakazi wa kata ya Komolo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya, ambaye pia ni Mbunge wa Simanjiro amesema Saning'o atawatumikia na kuwaunganisha wakazi wa Kata ya Komolo,
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer amesema Saning'o ni kiongozi jasiri na mbunifu ambaye atawaongoza vyema wana Komolo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Wambura Igembya amewapongeza wakazi wa Komolo kwani wana msimamo na walimuahidi ushindi kwa nafasi ya udiwani, ubunge na Rais.
Mchungaji na mwimbaji Agostino Laizer amemwekeza Saning'o kuwa kiti alichokalia siyo cha starehe wala cha raha ni kiti cha kutatua kero, matatizo na changamoto za watu wa Komolo.
MWISHO

No comments:
Post a Comment