Na Mwandishi wetu, Mirerani
maipacarusha20@gmail.com
CHAMA cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) kimenunua kiwanja cha thamani ya Sh30 milioni kwa ajili ya ujenzi wa matumizi ya ofisi na ukumbi wa mikutano.
Chama hicho cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara hakina ofisi ambayo ni mali yao hivyo kupitia kiwanja hicho watajenga ofisi zao na ukumbi wa mikutano.
Mwenyekiti wa Marema, Elisha Nelson Mnyawi ameyasema hayo kwenye mkutano mkuu wa mwaka 2025 wa wanachama wa MAREMA, Tawi la Mirerani ambao wanachimba madini ya Tanzanite na kinywe.
Mnyawi amesema kwa sababu makao makuu ya MAREMA yapo Mirerani, wamenunua kiwanja hicho kwa ajili ya kujenga ofisi zao na ukumbi.
"Ninawashukuru Makamu Mwenyekiti Money Yusuf, kampuni ya California, Joseph Manga na mimi mwenyewe kwa kutoa Sh5 milioni kila mmoja kwa ajili ya kununua kiwanja hicho," amesema Mnyawi.
Amesema lengo ni kuhakikisha MAREMA inakuwa na ofisi yake na kila tawi linakuwa na ofisi zake kwa lengo la kuwatumikia wachimbaji madini wa Manyara.
Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Mirerani, Peter Laizer amewapongeza wachimbaji madini kwa kupisha kanuni ya kuchangia chama chao kwa kutoa asilimia moja ya mapato yao baada ya uzalishaji.
"MAREMA ni taasisi kubwa hivyo kitendo cha wachimbaji kupitisha kanuni ya kuchangia chama chao kinapaswa kupongezwa kwani wataweza kujiendesha wenyewe," amesema Laizer.
Katibu wa MAREMA Tawi la Mirerani Rachel Njau ameipongeza kampuni ya Franone mining LTD kwa kuamua kujenga zahanati kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite ili kutoa huduma za afya kwa wachimbaji.
"Tunaishukuru Franone kwa hilo kwani tayari Wizara ya Madini imeshatuonyesha eneo la ujenzi wa zahanati hiyo na tunatarajia kazi ya ujenzi itaanza wakati wowote kuanzia sasa," amesema Njau.
Mmoja kati ya wachimbaji madini ya Tanzanite, Hamis Kim amesema suala la ruzuku za serikali kutolewa kwa wachimbaji linapaswa kuangaliwa upya ili waongezewe nguvu.
"Miaka iliyopita Serikali kupitia Wizara ya Madini, ilikuwa inatoa ruzuku kwa wachimbaji ila hivi sasa suala hilo limesitishwa hivyo wachimbaji kuwa na wakati mgumu katika uchimbaji," amesema Kim.
MWISHO

No comments:
Post a Comment