![]() |
| Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA Mussa Kuji akizungumza na waandishi wa Habari |
![]() |
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) leo Desemba 25, 2025 amezungumza na vyombo vya habari kuhusu ajali ya helikopta iliyotokea tarehe Desemba 24, 2025 majira ya saa 11:30 jioni katika eneo la Barafu, Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Kuji alieleza kuwa helikopta ya kampuni ya Kilimeda Air iliyokuwa ikifanya shughuli za uokoaji ilianguka na kusababisha vifo vya watu watano (5), wakiwemo mwanamke mmoja na wanaume wanne (4).
Kamishna Kuji alitaja majina ya waliofariki kuwa ni Costantine Mazonde (42), raia wa Zimbabwe, rubani wa helikopta na mkazi wa Soweto, Manispaa ya Moshi; David Plos (30), mtalii na raia wa Jamhuri ya Czech ; Anna Plosova (30), mtalii na raia wa Jamhuri ya Czech; Jimmy Daniel (32), daktari wa kampuni ya Kilimeda Air na mkazi wa Rau, Moshi; pamoja na Innocent Mbaga (35), muongoza watalii na mkazi wa Moshi.
Aidha, Kamishna Kuji alieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana, TANAPA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Anga pamoja na mamlaka nyingine husika zinaendelea na uchunguzi wa kina wa tukio hilo. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Taratibu za kukabidhi miili ya marehemu zinafanyiwa kazi kwa kuzingatia taratibu na miongozo mbalimbali, ikiwemo mawasiliano na Ubalozi wa Jamhuri ya Czech na Zimbabwe kwa wageni, na kwa wale wa ndani taratibu za mawasiliano na familia zao zikiendelea.


No comments:
Post a Comment