![]() |
| RAIS Samia Suluhu Hassan akizungumza na wazee wa Dare es Salaam mapema leo |
Na Mwandishi Wetu Maipac
maipacarusha20@gmail.com
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Dar es Salaam, Salum Matimbwa amesema wamefadhaishwa na matukio ya vurugu za Oktoba 29, mwaka huu na kwamba wamefurahishwa na hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuonyesha kuchukizwa nayo.
Ametumia jukwaa hilo kurejea historia ya kuwepo kwa kodi ya kichwa nchini, iliyochukiwa na wengi enzi hizo, akisema hakuna aliyeingia barabarani kuandamana, badala yake Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliongoza mazungumzo hadi mambo yakabadilika.
Mzee Matimbwa ameyasema hayo leo, Jumanne Desemba 2, 2025 alipozungumza katika mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na wazee wa Jiji la Dar es Salaam.
Amesema vurugu zilizotokea zimewastua na kuwafadhaisha kwa sababu zimeambatana na vifo, mali za watu zimeharibiwa na miundombinu inayosaidia watu imeathiriwa.
“Kwa kweli imetufadhaisha. Wazee tumesikitishwa na vifo vilivyotokea na uharibifu huo na tunamuomba Mungu awahifadhi wale waliotangulia na awaweke mahali pema wanapostahili,” amesema.
Hata hivyo, ameeleza kufurahishwa na hatua ya Rais Samia kuonyesha kuchukizwa na matukio hayo na kauli yake ya kurudisha amani.
Amesema wakati nchi inatawaliwa na wakoloni, kulikuwa na kodi ya kichwa na isingewezekana kutoka eneo moja kwenda lingine kama haujalipa.
Pamoja na yote hayo, amesema hakuna aliyeingia barabarani, bali Mwalimu Nyerere aliongoza mazungumzo na hatimaye yote yamekwisha, ndio maana kwa sasa wanashangaa yaliyotokea imekuaje.
Amesema Tanzania kitambo imekuwa kisiwa cha amani na hawana shaka chini ya uongozi wa Rais Samia hilo litadumu.




No comments:
Post a Comment