![]() |
| WAZIRI wa Madini, Anthony Peter Mavunde |
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
maipacarusha@gmail.com
WAZIRI wa Madini, Anthony Peter Mavunde, ameipongeza kampuni ya Franone Mining LTD na God Charity kwa kufanya shughuli za kijamiii (CSR) kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Waziri Mavunde ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani kuhusiana na wachimbaji kusaidia jamii.
Ameeleza kwamba kampuni ya Franone imejitolea kujenga zahanati kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite ambayo itakuwa inatoa huduma ya afya na tiba kwa wachimbaji.
Pia, amempongeza God Mwanga mkurugenzi wa kampuni ya God Charity kwa kujitolea kisima cha maji ili kitumike kwa ajili ya shughuli za wachimbaji wengine wa madini ya Tanzanite.
"Nawapongeza Franone na God Charity kwa kujitolea kusaidia wachimbaji wenzao kwa kujenga zahanati na kujitolea kisima, tunashukuru sana kwa hayo," amesema Waziri Mavunde.
Awali, mkurugenzi wa Franone mining, Onesmo Mbise alijitolea shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa zahanati katika machimbo ya madini ya Tomarini ya kijani eneo la Lemshuku kata ya Komolo Wilayani Simanjiro.
Akizungumza baada ya Waziri Mavunde kumuomba achangie vifaa vya ujenzi na fedha za kumlipa fundi, Mbise alikubali kwa kuchangia shilingi milioni 10 za zahanati hiyo.
"Mheshimiwa Waziri kwa upande wangu mimi nimekulia hapa Lemshuku kwa hiyo nitachangia shilingi milioni 10 katika ujenzi wa zahanati hiyo," amesema Mbise.
MWISHO

No comments:
Post a Comment