![]() |
![]() |
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
maipacarusha20@gmail.com
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema watumishi wa ajira mpya 8,416 kati ya 12,000 zilizoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan wamepangiwa vituo vyao vya kazi.
Aidha Waziri Kikwete amesema kati yao, wameshaanza kulipwa mshahara kama ambavyo Rais Samia alivyoelekeza kuwa watumishi wapya watakaowahi kuripoti vituoni kabla ya Januaria mwishoni waingizwe moja kwa moja kwenye mfumo wa mshahara.
Waziri Kikwete ametoa kauli Ijumaa Januari 30,2026 jijini Dodoma akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Dkt Samia na mafanikio yake ndani ya siku 100 katika muhula wake wa pili wa uongozi.
![]() |
Katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 Dkt Samia alitoa ahadi mbalimbali ikiwemo ajira mpya 12,000 za elimu na afya, akiahidi Watanzania kuwa zitatekelezwa ndani ya siku 100 katika utawala wake.
Katika mkutano huo, Waziri Kikwete amesema, “Ninayo furaha kuwajulisha kuwa watumishi 735 walioripoti kabla ya kufunga orodha ya mshahara waliingizwa mfumo wa malipo ya Serikali na wameshapata mishahara yao,” amesema Waziri Kikwete.
Waziri Kikwete ameongeza kuwa, watumishi wote wataingizwa katika mfumo wa mshahara wa Serikali kwa kadri walivyoripoti katika vituo vyao vya kazi.
Kwa mujibu wa Waziri Kikwete, kati ya watumishi hao 8, 416 walioripoti vituoni ni 3,694 wanatoka kada ya elimu na 4,722 kada ya afya ambao wapo katika halmashauri mbalimbali.
Waziri Kikwete amesema waombaji waliopenya katika usaili katika idadi ya 12,000 wanaendelea kupewa barua zao ili kuripoti katika vituo vyao vya kazi.



No comments:
Post a Comment