Na Mwandishi wetu, Simanjiro
maipacarusha20@gmail.com
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Samwel Warioba Gunza ameachiwa huru na mahakama kwenye kesi ya rushwa ya shilingi milioni 5 na matumizi mabaya ya madaraka.
Hata hivyo, aliyekuwa DED huyo wa Simanjiro, Gunza hakuwepo mahakamani kwani yupo magereza bado anatumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa kesi nyingine ya rushwa alipohukumiwa mwaka 2025.
Katika kesi hiyo, Gunza alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Simanjiro, Onesmo Nicodemo na kusomewa shitaka na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU).
Katika hukumu ya shauri hilo la uhujumu uchumi lililosomwa kwenye mahakama hiyo iliyopo mji mdogo wa Orkesumet, Gunza hakukutwa na hatia.
Hakimu Nicodemo akisoma hukumu hiyo ameieleza mahakama hiyo kuwa hakukuwa na ushahidi usiokuwa na mashaka wenye kumtia hatiani mshtakiwa huyo, katika makosa mawili ya rushwa na kutumia madaraka vibaya.
Amesema katika shtaka la kwanza mshtakiwa huyo alishtakiwa kuwa akiwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro alitumia fedha za halmashauri hiyo kiasi cha shilingi milioni 5 kwa matumizi yake binafsi.
Amesema Gunza alishtakiwa kwa makosa ya ufujaji na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 (1) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa, sura ya 329 R.E 2022.
Hakimu Nicodemo ameeleza kwamba katika shtaka la kwanza Gunza hakutiwa hatiani kwani hakukuwa na ushahidi usiotia shaka kuwa alichukua Sh5 milioni za halmashauri hiyo kwa ajili ya matumizi yake bnafsi.
Ameeleza kwamba kutokana na kutotiwa hatiani na shataka la kwanza, hivyo shtaka la pili la kutumia madaraka yake vibaya halina uzito tena hivyo anaachiwa huru hana hatia.
Hata hivyo, Gunza hakuwepo mahakamani hapo wakati wa hukumu hiyo kwani yupo magereza anatumikia kifungo cha miaka 20 jela alipohukumiwa na mahakama hiyo mwaka 2025.
Katika kesi ya awali iliyomtia hatiani mwaka 2025, mbele ya hakimu Charles Uiso wa mahakama ya wilaya ya Simanjiro, Gunza alitiwa hatiani kwa makosa ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na kuhukumiwa kwenda jela miaka 20.
Gunza alitiwa hatiani kwa kosa la kutoa zabuni ya kukusanya ushuru bila kufuata utaratibu na kanuni za halmashauri hiyo na kutumia madaraka yake vibaya kwa manufaa yake.
MWISHO

No comments:
Post a Comment