Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
MAJONZI na hasira vimeibuka katika kijiji cha Bwakila Chini, kata ya Bwakila wilayani Morogoro, baada ya wananchi kukataa vikali uamuzi wa Serikali ya Wilaya wa kuwaruhusu kulima maeneo yenye mgogoro kwa muda wa mwaka mmoja tu, wakidai ni njia ya kuzima madai yao ya msingi ya ardhi na migogoro baina ya wananchi na Viongozi wa kijiji.
Kauli ya mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, Hilary Sagala, kuwa mwekezaji Morogoro Sugar ameridhia wananchi kulima kwa mwaka mmoja, ilizua makelele na minong’ono katika mkutano wa hadhara, uliofanyika ofisi za kijiji ambapo pia kuna ofisi ya Kata, wananchi wakidai wanataka majibu ya tume iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya na si ruhusa ya muda.
“Hatuhitaji fadhila ya mwekezaji, tunahitaji haki ya ardhi yetu,” alisema mmoja wa wananchi. Kulwa Malunga.
Akasema uamuzi huo hauna tofauti na kuchelewesha mgogoro.
“Tume iliundwa, ikafanya kazi, sasa tulitegemea mkutano huu upewe majibu ya kile walichobaini na maamuzi halali kulingana na ukweli wa suala hili, vinginevyo hakukuwa na haja ya mkutano huu” aliongeza.
Machungu zaidi yalijitokeza kwa Victoria Francis aliyedai kunyimwa fidia licha ya kutoa kwa hiyari eneo lake kwa mwekezaji Morogoro sugar, huku watu wengine wakilipwa na kijiji fedha za fidia zilizotolewa na mwekezaji kwa mgongo wa ardhi yake.
“Wanakula mamilioni yasiyowahusu, mimi mtoto wangu alikuwa anauwa,tukalazwa,nyuma viongozi wa kijiji wakapeleka watu wengine wasio na ardhi kujiandikisha kwenye eneo langu, wakasema nikafungue akaunti waniwekee hela zangu lakini hadi leo wananizungusha na karatasi za kufungua akaunti hizi hapa"Alisema huku akilia na kumpa mwakilishi wa mkuu wa wilaya karatasi za benki alizofungulia akaunti.
![]() |
Mkazi mwingine Said Hamad alisema mgogoro huo umejaa tuhuma nzito ikiwemo ardhi kugawiwa watu wasio wamiliki, kutokuitishwa mikutano, kukosekana taarifa za mapato na matumizi na viongozi wa kijiji kuwa watuhumiwa kwenye sakata hilo.
“Hadi sasa Kijiji hakina uongozi halali tangu afungiwe ofisi na wananchi na Mkuu wa wilaya Kumsimamisha Mwenyekiti kupisha uchunguzi, lakini maamuzi bado yanatolewa kana kwamba hakuna tatizo,” alisema.
Jeshi la Polisi kupitia SSP Denis Mujumba lilionya wananchi kutochukua sheria mkononi, likisisitiza kuwa yeyote atakayokiuka sheria katika kupinga maamuzi hayo atachukuliwa hatua.
Akizungumza kama mjumbe wa kamati ya usalama ya wilaya, akawataka wananchi kuwa na subira wakati maamuzi mengine yanaendelea kufanyiwa kazi na ofisi ya wilaya ikiwemo yanayohusu tuhuma za jinai na nyinginezo.
Hata hivyo, viongozi wa tume wanaotokana na wananchi walisema wanaamini Serikali ya Rais Samia ni sikivu, mkuu wa wilaya pia ana Busara hivyo wataona tatizo lililopo kijijini hapo na haki itendeke.
“Majibu ya tume ni haki ya wananchi. Bila uwazi, mgogoro huu utaendelea,na hapa hatukupewa nafasi kuzungumza lakini, ni mengi tumebaini na kushauri lakini leo tunaambiwa eti mwekezaji karidhia tupewe mwaka mmoja tulime, wakati huyu huyu analalamikiwa kuchukua maeneo bila kufuata taratibu” akaongeza Katibu wa tume upande wa wananchi Salum Kassim.
Naye Mwenyekiti wa tume, Abuu Silia, alisema bado wanaimani Mkuu wa wilaya atakwenda kuweka wazi yaliyobainika kwenye tume na kuchukua maamuzi sahihi kwani wananchi watashindwa kujipanga kufanya mipango endelevu ya kilimo ya muda mrefu kutokana na vikwazo vilivyopo.
![]() |
Septemba mwaka jana Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala aliunda tume ya wananchi 10 ambao alidai wangeshirikiana na wataalamu na wadau wengine ambao wangeteuliwa wakiwemo kutoka halmashauri na ofisi ya wilaya, kuchunguza mgogoro wa ardhi, tuhuma za Mwenyekiti na madai mengine yaliyosababisha wananchi kufunga ofisi ya kijiji, wakimkataa mwenyekiri Hemed Mvunyo.
Ingawa DC alionya kwa kitendo hicho cha kufunga ofisi kuwa ilikuwa ni jinai na kutaka wasirudie wakati mwingine hata kama wanadai wanachoamini ni haki zao.
Mwisho.




No comments:
Post a Comment