Na Queen Lema,Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kutekeleza dhamira yake ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, baada ya kuzindua rasmi huduma za vipimo na matibabu ya magonjwa ya moyo bila malipo katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (Seliani), kwa ushirikiano na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza wakati wa kukagua utekelezaji wa mpango huo leo Januari 6, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha huduma za kibingwa zinapatikana katika maeneo yote ya nchi bila wananchi kulazimika kusafiri umbali mrefu.
“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa uwekezaji huu wa kimkakati. Huduma hizi zitawaokoa wananchi wengi ambao awali walishindwa kupata matibabu kutokana na gharama na umbali,” alisema Makalla.
Makalla aliongeza kuwa zaidi ya wananchi 1,200 tayari wamenufaika na huduma za moyo tangu kuanzishwa kwa kituo hicho, akibainisha kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa watu wasiokuwa na uwezo ili waweze kupata matibabu au rufaa kwenda JKCI jijini Dar es Salaam bila vikwazo.
Aidha, alisisitiza kuwa uwepo wa kituo hicho utakuwa na mchango mkubwa katika maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, kwani Mkoa wa Arusha utakuwa mwenyeji wa wageni na washiriki, hivyo kuwa na huduma bora za afya ni hatua muhimu ya kulinda afya za wote.
Wananchi waliopata huduma hizo wameelezea furaha na shukrani zao kwa Serikali, wakisema mpango huo umewasaidia kupunguza gharama na muda wa kutafuta matibabu nje ya mkoa.
“Huduma hizi ni baraka kubwa kwetu. Zamani tulikuwa tunalazimika kwenda Dar es Salaam, lakini sasa tunapata matibabu hapa hapa Arusha,” alisema Bi. Rehema Mollel, mkazi wa Olasiti.
Naye Bw. Joseph Laiser, mkazi wa Monduli, alisema: “Madaktari wametupokea vizuri, vipimo ni vya kisasa, na hakuna malipo. Huu ni ukombozi kwa wananchi.”
Makalla pia alitumia nafasi hiyo kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote (UHC), akieleza kuwa bima hiyo itasaidia kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa gharama nafuu na kwa wakati, sambamba na kupunguza utegemezi kwa Serikali pekee.
Kwa upande wa wataalamu wa afya, wamesema huduma hizo zitaongeza uelewa kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa moyo mapema, hatua ambayo itapunguza vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza nchini. Wameahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wote watakaofika kupata matibabu.
Programu ya vipimo na matibabu ya magonjwa ya moyo bure inaendelea kutolewa katika Hospitali ya Seliani, na matarajio ni kuwafikia wananchi wengi zaidi ndani ya Mkoa wa Arusha na kanda nzima ya Kaskazini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Serikali ya kujenga Taifa lenye wananchi wenye afya bora na uchumi imara.


No comments:
Post a Comment