![]() |
Na Mwandishi wetu, maipac
maipacarusha20@gmail.com
Ilianza ahadi, ikafuata mipango na mikakati, hatimaye Watanzania kwa mara ya kwanza katika historia, watanufaika na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (BAW), utakaoanza kutekelezwa Jumatatu Januari 26, 2026 kwa awamu ya kwanza.
Kuanza kwa mpango huo wa bima ya afya kwa wote, ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, aliposema ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa atalitekeleza jambo hilo.
Hatua ya kuanza utekelezaji wa bima hiyo, inatarajiwa kuwaondolea mzigo wa gharama za matibabu wananchi wasio na uwezo wakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu, ambao gharama zao zitabebwa na Serikali.
Taarifa kuhusu kuanza kwa utekelezwaji wa bima hiyo, imetolewa jijini Dodoma leo, Ijumaa Januari 23, 2026 na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wakati wa kikao kazi cha kitaifa cha utekelezaji wa bima ya afya kwa wote.
Amesema awamu ya kwanza ya utekelezaji itaambatana na kuanza kutumika kwa kitita cha huduma muhimu, kitakachotolewa na skimu za bima ya afya, wakilenga makundi yaliyohatarini ili kupata huduma za afya bila kikwazo cha fedha.
"Bei ya kitita hicho ni Sh150,000 kwa kaya isiyozidi watu sita, kikiwa kinazingatia utaratibu wa rufaa katika vituo vya afya vilivyoingia mkataba na Skimu za Bima ya Afya.
"Nasisitiza kuwa Bima ya Afya kwa Wote si mradi wa wizara moja bali ni ahadi ya Taifa kwa wananchi wake. Mafanikio ya mpango huo yatapimwa si kwa hotuba wala maagizo, bali kwa idadi ya wananchi wanaolindwa dhidi ya gharama za matibabu na wanaopata huduma kwa heshima," amesema.
Amewataka wakuu wa mikoa yote nchini, kubeba dhamana ya moja kwa moja, binafsi na isiyohamishwa ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote katika mikoa yao.

No comments:
Post a Comment