WANAFUNZI WA CHUO KIKUU (MUM) WASISITIZA KUDUMIA AMANI NDANI YA NCHI. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 14 January 2026

WANAFUNZI WA CHUO KIKUU (MUM) WASISITIZA KUDUMIA AMANI NDANI YA NCHI.

 




Na Lilian Kasenene ,Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM) wamewashauri Watanzania hususani vijana kuendelea kudumia amani kwa vile ina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo yakiwemo kwa wanafunzi kusoma bila bughudha.


Mtoa Mafunzo Msaidizi wa Chuo Kikuu hicho ,( Tutorial Assistance ) Hussein Mohamedi Hassani alisema hayo  katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi wakati aliambatana na baadhi ya viongozi wa serikali ya wanafunzi na wanafunzi ili  kufanya utalii wa ndani na kimafunzo, hivi karibuni.


Hassani alisema kuwa elimu  wanayoipata wanafunzi katika ngazi mbalimbali inaenda sambamba na uwepo wa masuala ya kudumishwa kwa amani  ndani ya nchi kwani  ni kitu cha kwanza kwa binadamu ili aweza kupata maendeleo yake ya kijamii na kiuchumi.


Alisema kuwa amani ni jambo la msingi wa kila kitu ,ni msingi wa maendeleo ya kila mmoja wetu ndani ya jamii kwenye  nyanja za  kiuchumi, kijamii , kisiasa na kiimani.


 “ Tunabudu, tunaishi kwa sababu ya amani, tunasoma kwa sababu tuna amani ,watanzania na dunia kwa ujumla tuendelee kupeana wosia ya kwamba tuendelee kudumisha amani ili kuweza kufikia malengo mazima ya Binadamu kuumbwa hapa Duniani” alisisitiza Hassani.


Alisema  wakiwa ni wasomi wa Chuo Kikuu hicho wanajivunia kuendelea na masomo  yao kutokana na amani iliyopo ambayo pia imewawezesha kufanya ziara ya utalii wa ndani na wa kimafunzo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.


Kwa upande wake  Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu hicho, Abubakari Maneno Yahaya alisema uongozi wao kwa kushirikiana na uongozi wa Kikuu cha Waislamu uliandaa safari ya kutembelea hifadhi hiyo ikiwa na lengo kuwawezesha wanafunzi wapya wa mwaka wa kwanza waifahamu vyema Morogoro.


Yahaya alisema si kuifahamu Morogoro pekee , bali ni pamoja na kupata ujuzi mbalimbali wakiwa katika hifadhi hiyo  na kwamba siku za usoni , Serikali ya wanafunzi itawaleta wanaosoma  masomo ya Arabic ili kuwasoma wanyamapori kwa kutumia lugha ya kiarabu .


“ Tumeambatana na timu ya watu 31  na wengi ni wanafunzi wapya wa mwaka wa kwanza , miongoni mwa faida ambayo tunaipata kutembelea hifadhini tukiwa watalii wa ndani tunaongeza pato la Taifa , pia ni  ziara ya kimafunzo kwani wapo wanafunzi wanaosoma Jiografia na Historia wataweza kuelewa mambo mbalimbali ya asili ya wanyamapori  “ alisema  Yahaya.


Nao baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu hicho akiwemo Matroni Sharifa Maulidi kwa nyakati tofauti walifurahishwa kuweza kutembelea hifadhi hiyo na kujionea aina mbalimbali ya wanyamapori mbashara na kujifunza masuala ya maisha yao wakiwa hifadhini.


Mwisho.

No comments: