![]() |
| Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Nyerere Ephraim Mwangomo |
Na Said Njuki, Maipac
maipacarusha20@gmail.com
TANZANIA imebarikiwa rasilimali za kutosha, yakiwepo madini, mito, maziwa, bahari na hata misitu yenye uoto wa asili, lakini pia wamo ndege na wanyamapori wa aina mbalimbali.
Kutokana na kuwemo kwa rasilimali hizo lukuki, Serikali ililazimika kuanzisha mamlaka mbalimbali likiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ili kuhifadhi rasilimali hizo kwa faida ya vizazi vijavyo na Taifa kwa ujumla.
Jumla ya hifadhi 21 nchini zipo chini ya TANAPA ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Nyerere yenye ukubwa wa kilomita za mraba 29,276 ambayo ndiyo hifadhi kubwa zaidi barani Afrika kwa sasa.
Rasilimali hizo ni vivutio adhimu vinavyovitoa watalii wengi wa nje, wakazi na wazawa na kulipatia Taifa pato linalokuwa nyenzo kubwa katika kusukuma maendeleo ya taifa.
Tukisimama katika kipengele cha utalii, wakati lengo la Taifa ni kupokea watalii zaidi ya milioni nane ifikapo mwaka 2030, utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere umezidi kupaa siku hadi siku.
Katika kupanda huko kwa idadi ya watalii wageni, walazi na wazawa, vivyo hivyo na pato la hifadhi hiyo nalo linakuwa kwa kasi kubwa.
Kamishna Msaidizi wa Hifadhi hiyo, Ephraim Mwangomo anasema jumla ya watalii 47,974 wameingia hifadhini mwaka 2024/2025 na kukusanya jumla ya shilingi bilioni 13.88
Akiongea na waandishi wa habari Makao Makuu ya Hifadhi hiyo Matambwe alisema idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na idadi ya watalii waliotembelea Hifadhi hiyo mwaka 2023/2024 ambao ni 45,682, makusanyo yakiwa ni shilingi bilioni 11.9.
Alisema takwimu miaka sita iliyopita zinaonyesha mwaka 2019/2020 walipokea wageni 151 na kukusanya shilingi milioni 51,538,800, mwaka 2020/2021 wageni 15,850, makusanyo shilingi bilioni 3.1, mwaka 2021/2022 wageni 21,655, makusanyo shilingi bilioni 5.56 na mwaka 2022/2023 wageni 40.490 na kukusanya shilingi bilioni 20.94.
"Utaona ni kwa kiasi gani utalii unavyopanda kwa kasi katika hifadhi yetu na kupandisha pato letu kwa kasi kubwa...haya yote yanatokana ubora wa hifadhi yetu lakini pia huduma safi zinazopatikana hifadhini". alisema Kamishna Mwangomo.
![]() |
Muhifadhi Mwandamizi kitengo cha utalii, Themistocles Bitta alisema ongezeko hilo ni kielelezo cha kupaa kwa kasi kwa utalii katika Hifadhi hiyo.
"Ni jambo la kujivunia ndani ya miaka sita tu tumetoka katika idadi ya watalii 151 mwaka 2029/2020 hadi 47,974 mwaka 2014/2025 na pato kuongezeka kutoka shilingi milioni 51.5 mwaka 2019/2020 hadi shilingi bilioni 13.88 mwaka 2024/2025".Alisema Bitta.
Hifadhi ya Nyerere yenye ukubwa wa kilomita za mraba 29,276 inakadiriwa kuwa na wingi wa wanyama wengi wakiwemo nyati 60,000 viboko 29,000 na twiga 1,700.
Hifadhi hii ndipo lilipo bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) na bwawa la kimkakati la Kidunda ambalo linatarajiwa kufuta kabisa adha ya maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani hapo litakapokamilika.
![]() |





No comments:
Post a Comment